WAZIRI wa madini na uchumi wa baharini Ali Hassan
Joho amesisitiza kwamba kauli zake ni sawa na tamko la serikali pindi
anapozungumza popote.
Akizungumza katika kaunti ya Tana River katika
shughuli ya Danson Mungatana, waziri Joho alifafanua kauli ya naibu rais
Kithure Kindiki kuhusu jinsi serikali imerahisisha maisha ya mwananchi wa
kawaida katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Joho akiunga mkono kauli za naibu wa rais,
alisisitiza kwamba maadamu yeye sasa ni waziri, anapozungumza ni sawa na
serikali imezungumza.
“Mheshimiwa
naibu wa rais amesema hapa kwamba anataka yeye na rais wetu William Ruto
kuhakikisha kwamba wanaweka pesa mifukoni mwa watu. Mnajua mimi ni waziri sasa
hivi. Ama hamuelewi hilo? Mimi nikiongea hapa, mimi ni serikali kamili. Lazima tuweke
mipango ya kuwaelewesha,” Joho alisema.
Joho alichukua fursa hiyo kuelezea majukumu yake
katika wizara ambayo alirithi kutoka kwa Salim Mvurya ambaye hivi majuzi
amehamishiwa tena katika wizara ya michezo na Sanaa.
“Mimi
binafsi katika wizara yangu ambayo nimerithi kutoka kwa ndugu yangu Salim
Mvurya, kuna mambo ya uvuvi, madini, na uchumi wa baharini. Hapa mimi nataka
tukubaliane kwamba tumesikilizana na mheshimiwa Ali Wario barabara itakuja hapa
ili wavuvi wetu wakivua samaki wanapata soko,”
Joho alijipigia debe.
Kauli ya gavana huyo wa zamani wa Mombasa inajiri
wiki chache baada ya kuvutia maoni kinzani mitandaoni kutokana na kauli zake za
kuwashambulia kwa maneno wanaharakati wa mitandaoni wanaokosoa serikali.