Idara ya utabikri wa hali ya hewa nchini imetangaza kuwa hali ya mvua itapungua kwa viwango vikubwa katika maeneo mengi nchini kuanzia Disemba 26, majira ya joto na jua yakianza kushuhudiwa.
Kwa mujibu wa utabiri huo uliotolewa Jumatatu Disemba 23, baadhi ya maeneo bado yatashuhudia mvua ikiwemo sehemu za magharibi mwa nchi, maeneo ya kati ya milima, sehemu zilizo kando ya ziwa Victoria, maeneo ya kati na kusini mwa bonde la ufa, sehemu za nyanda za chini za kusini mashariki mwa nchi na baadhi ya sehemu za pwani za Kenya.
Vile vile, vipimo vya joto vinatarajiwa kupanda haswa wakati wa mchana vipimo vya juu zaidi vikitarajiwa kuzidi Zaidi ya nyuzi 30.
Sehemu za pwani, kaskazini mashariki pamoja na maeneo ya magahribi pia inatarajiwa kupokea ongezeko la juu la joto. Idara ya hali ya hewa nchini imewataka wakaazi katika sehemu zitakazorekodi joto la hali ya juu kunywa maji mengi kwa ajili ya afya yao.
Hata hivyo, wakaazi wa maeneo ya kati mwa nchi na kusini mwa bonde la ufa wametakiwa kujitayarisha kwa usiku wenye nyuzi za chini mno za joto ambazo idara ya hali ya hewa imetabiri kuwa huenda zikafika chini ya nyuzi 10. Baadhi ya sehemu ambazo zinatarajia baridi wakati wa usiku ni nyanda za chini za kusini mashariki, maeneo ya kati ya nchi na kusini na kati ya bonde la ufa.
Idara ya hali ya hewa imewashauri Wakenya kupanga shughuli
zao ipasavyo ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.