ERIC WAMUMBI, Mbunge wa Mathira, ambako ni Eneobunge la aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua ameibua madai mapya dhidi ya kiongozi huyo akimhusisha na msururu wa utekaji nyara wa vijana kadhaa humu nchini.
Katika barua aliyoiandikia idara ya DCI, Wamumbi alimtuhumu
mtangulizi huyo wake katika Eneobunge la Mathira kwa kuhusika katika kuwateka
nyara vijana na kisha kuwaficha katika mgahawa wa kifamilia wa Olive Gardens
jijini Nairobi.
Wamumbi aliitaka DCI kuanzisha uchunguzi dhidi ya
shughuli zinazofanyika katika mgahawa huo, akidai kuwa huenda vijana
wanaoripotiwa kupoteza wanafichwa katika hoteli hiyo.
“Ninaandika
kuomba uchunguzi dhidi ya shughuli zinazofanyika katika mgahawa wa Olive
Gardens Nairobi, kuhusiana na utekaji nyara unaoendelea. Uku tukiendelea
kuhuzunika na wazazi ambao wako na wasiwasi kuhusu waliko wanao, ninaamini
baadhi ya watu wanafanya mikutano katika hoteli hiyo wakipanga utekaji nyara feki
ambao unanuia kuchochea umma,” Barua ya Wamumbi
ilisoma.
Aliendelea kwa kumtag Gachagua na kumtaka kuachilia
vijana ambao alimtuhumu kuwateka nyara, akisema kwamba yeye ni baadhi ya watu
wanaomjua vizuri sana naibu rais huyo wa zamani.
“H.E.
Rigathi Gachagua, EGH, Waachilie watoto wote ambao umekuwa ukiwashikilia kwenye
hoteli ya Olive Gardens na ukomeshe mchezo wa kuigiza. Wale wa kijijini kwako
tunakujua na maigizo. Wacha kutesa wazazi sababu ya siasa bwana,”
Wamumbi aliongeza.
Barua yake kwa DCI inajiri siku chache tu baada ya
baadhi ya viongozi akiwemo mbunge wa Kikuyu ambaye pia ni kiongozi wa wengi
katika bunge, Kimani Ichung’wah na katibu wa muungano wa wafanyikazi COTU,
Francis Atwoli kudai kwamba baadhi ya vijana wanajificha wakidai kutekwa nyara.
Wiki iliyopita, Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi
Mutuse pia alitoa taarifa sawia na hiyo akidai kwamba utekaji nyara unaoendelea
unafanywa na Rigathi Gachagua.
Hata hivyo, ni madai ambayo Gachagua ameyapinga
vikali akisema kwamba serikali ina wajibu wa kulinda kila Mkenya na kukomesha
visa vya vijana kutoweka.