Maafisa wa ujasusi wanamzuiliwa jamaa mmoja mwenye umri wa miaka 30, aliyepatikana na vitambulisho vya kitaifa vya watu vilivyopotea, simu 10 bandia na idadi ya maganda ya kuhifadhi laini za simu.
Kukamatwa kwa mshukiwa huyo kunajiri baada ya msako wa siku kadhaa uliondeshwa na maafisa wa usalama wakimtafuta mshukiwa huyo anayedaiwa kutekeleza wizi katika gari moja mnamo Januari 3.
Katika msako kwenye nyumba ya mwanamume huyo bidhaa hizo zilipatikana zikiwa chini ya umilisi wa mshukiwa katika mtaa wa Hilton viungani mwa eneo la Ruiru.
Uchunguzi wa maafisa wa polisi kupitia hojaji kwa mshukuwa umebaini kwamba jamaa huyo amekuwa akitumia vitambulisho vya kitaifa vya watu mbali mbali kusajili akaunti kadhaa kwenye jukwaa la biashara la mtandaoni.
Pia, ilibainika kuwa akaunti ghushi zinazosajiliwa na mshukiwa uyo hutumika kuwalaghai Wakenya mtandaoni kwa uwongo wa kuwauzia bidhaa za simu ambazo huwa ghushi.
Ulaghai unaoendeshwa na mshukiwa huyo ambaye sasa yuko mikononi mwa maafisa wa polisi, huwasababishia ukosefu wa amani watu wengine ambao kwa uhalisia hawakuhusika kwenye ulaghai bali ni vitambulisho vyao vilivyopotea hutumika kuendesha ulaghai huo.
Hata hivyo wapelelezi wanaamini kuwa walalamikaji zaidi
waliokubali hila za mshukiwa wako nje, na wanaitwa kuripoti kituoni ili
kurekodi kauli zao.
Mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi
cha Ruaraka wakati upelelezi zaidi ukiendelea.