RAIS WILLIAM Ruto sasa ameibuka na madai mapya kuhusu mwenendo wa baadhi ya vijana wanaotumia mitandao ya kijamii kutengeneza picha za baadhi ya viongozi kwenye majeneza na makaburi.
Akizungumza wakati wa
kuzindua chuo anuwai cha Ngeria TTI katika kaunti ya Uasin Gishu, kiongozi wa
taifa alisema vijana wengi wanafaidika kutoka kwa matumizi mazuri ya mitandao
ya kijamii na utandawazi, huku akiwasuta wale wanaotumiwa vibaya kueneza chuki
na propaganda dhidi ya viongozi wa nchi.
Ruto alisema kwamba kuna
baadhi ya wanasiasa ambao sasa wanawalipa vijana wenye ujuzi wa kutumia akili
mnemba (AI) kutengeneza picha za viongozi wakiwa kwenye majeneza na makaburi.
“Mimi nawauliza vijana
wale wengine, wasipotoshwe na wanasiasa wa kuwalipa pesa kidogo eti waweke
picha za viongozi eti kwenye makaburi. Mimi nataka niwaambie hawa vijana, leo
mtaweka viongozi kwenye kaburi kesho mtaweka wazazi wenu kwenye kaburi na
keshokutwa mtaweka wenzenu, marafiki zenu na siku nyingine ni nyinyi mtaanza
mambo ya mauaji,” Ruto alisema.
Rais pia alisema kwamba wale wanaowatia moyo
vijana kuendelea na hulka hiyo ya kuwakoshea heshima mitandaoni viongozi wao
kukoma mara moja kwani ni vizuri kuwafunza vijana tabia njema.
“Ningependa kuwaambia wale
wanaowaweka viongozi kwenye majeneza, kwamba ni lazima tuwaambie vijana kwamba
tabia njema hulipa. Badala ya kutumia mtandao kuweka picha za viongozi kwenye
majeneza, tumia mtandao kutengeneza pesa na kupata ajira kwenye nyinyi na
kuboresha maisha yenu,” rais aliongeza.
Mkuu wa taifa alisema
kwamba kwa sasa vijana wa Kenya zaidi ya 120,000 wanatengeneza pesa kutoka kwa
mitandao ya kijamii kutokana na matumizi mazuri ya mitandao hiyo.
“Ninajivunia sana vijana
ambao nimeona kwenye hii TVET, wale vijana ambao wanatengeneza pesa, wanaweka
pesa kwa mfuko, pesa ya madola kwa sababu ya kutumia intaneti, waweze kupanga
mambo yao ya ajira, na kuweza kufanya kazi le ya digital jobs. Na tuko na
vijana elfu 120 Kenya ambao tayari wanafanya kazi katika Digital jobs na kuweka
pesa zao kwa mfuko,” Ruto aliongeza.
Kiongozi wa taifa
atakamilisha ziara yake ya siku tatu Jumamosi katika ukanda wa Bonde la Ufa Kaskazini
ya siku tatu ambayo iling’oa nanga Alhamisi.