MBUNGE wa Dagoretti Kaskazini, Beatrice Elachi amewataka wanaodai kwamba Kenya inaelekea katika mkondo mbaya chini ya uongozi wa rais William Ruto kuondoka nchini.
Mbunge huyo ambaye
alikuwa akizungumza Jumapili katika ibada ya kanisa kwenye Eneobunge hilo,
ibada ambayo ilihudhuriwa na rais alisema kwamba amekuwa katika uwanja wa ndege
juzi na aliona jinsi watu wengi wana uchu wa kutoka nje wakitembelea Kenya.
Elachi alisema kwamba
aliona jinsi watalii wengi kutoka nje wamefurika uwanja wa ndege wakiwa na nia
ya kutalii Kenya na wakati uo huo kuna Wakenya wengi kwenye mitandao ya kijamii
wanateta kwamba Kenya ni mbaya.
Elachi aliwataka wale
wanaoteta kwamba Kenya ni mbaya kupoteza kutoka nchini kuliko kuchochea wengine
kuamini katika dhana hiyo.
“Ni lazima tutengeneze
uwanja wa ndege mheshimiwa rais. Nimekuwa huko juzi wageni wakitoka USA
madaktari. Watu walikuwa wamejaa nje, walikuwa wanaondoka na wengine wanaingia…”
“Wale wageni wanaingia
Kenya wanasema Kenya ni nchi nzuri, na Mkenya ako hapa anasema eti Kenya ni
mbaya. Kama Kenya ni mbaya si upotee! Kama Kenya ni mbaya unafanya nini hapa
mahali pabaya? Na kama hupotei basi ujue hii ni nchi yako na hakuna mahali
utaenda,” Elachi alifoka.
Mbunge huyo alisema
kwamba Mkenya akienda nchi yoyote kwa sasa watamkataa kwa vile watahisi kwamba
anaenda kuwaharibia nchi kwa vile nyumbani hawamheshimu rais wao.
“Ukienda Dar es Salaam
watakuangalia wanasema hawa Wakenya wanatusi mpaka viongozi wao, hawa wanakuja
kutuharibia nchi yetu. Sasa utaenda wapi?”
Elachi aliuliza.
Alitoa wito kwa Wakenya
kumheshimu rais Ruto, akisema kwamba kwa kufanya hivyo, watabarikiwa.
“Tulinde nchi yetu,
tuheshimu mheshimiwa rais. Na tukimheshimu tutabarikiwa ndio shilingi yetu
iimarike [dhidi ya sarafu za kigeni],” mbunge huyo wa
Dagoretti North alirai.
Wakati uo huo, kiongozi
wa taifa alisema kwamba anajihisi mwenye fahari kubwa kuwa rais wa Kenya,
akisisitiza kwamba ana wajibu mkuu kutoka kwa Mungu kubadilisha hii nchi.
Rais alitoa rai kwa
Wakenya kuunga serikali mkono katika jitihada zake za kuhakikisha uchumi wa nchi
unaimarika ili kurahisisha maisha ya Mkenya wa kawaida.