Sherehe zilizuka katika Shule ya Wasichana ya Lugulu iliyoko Bungoma baada ya Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC) kutoa matokeo ya shule hiyo ya KCSE 2024.
Hofu ilitanda kwa wazazi na wanafunzi baada ya KNEC kufutilia mbali alama za shule hiyo serikali ilipotangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne.
Matokeo ya muda yalionyesha watahiniwa 672 kati ya jumla ya 676 walipata alama C plus na zaidi, na kupata nafasi ya kuingia chuo kikuu moja kwa moja.
Shule ilipata daraja la wastani la 9.3417 mnamo 2024 ikilinganishwa na 9.3306 mnamo 2023. Shule hiyo ilikuwa na 13 A plain, 93 (A-), 191 (B+) 232 (B0, 118 (B-), 25 (C+), C (1), 1 (C-) na 2 (D+).
Hatua ya kuzuiwa kwa matokeo haikutarajiwa kwa shule ya Lugulu inayosifika kote nchini.
Mkuu wa shule, Dinah Cheruiyot pamoja na walimu walikuwa wametoa wito kwa watahiniwa wa KCSE wa 2024 na wazazi wao kuwa na subira.
“Ndugu Mzazi/Mlezi, tunafahamu kuwa mtoto wako bado hajapokea matokeo yake ya mitihani. Tafadhali uwe na uhakika kwamba suala hilo linashughulikiwa, na matokeo yatatolewa kwako kwa wakati ufaao. Mawasiliano zaidi yatafuata. Asante kwa subira na uelewa wako,” ilisoma barua iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Elimu Kanda ya Magharibi Jared Obiero.
Akizungumza wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCSE ya 2024, Waziri wa Elimu Julius Ogamba alitangaza kuwa matokeo ya watahiniwa 840 yamefutiliwa mbali kutokana na visa vilivyothibitishwa vya makosa ya mtihani.
Zaidi ya hayo, KNEC imezuia matokeo ya watahiniwa 2,829 kusubiri uchunguzi zaidi. Lugulu ni miongoni mwa shule zilizoathiriwa na kuzuiwa kwa matokeo.
Nyingine ni Shule ya Sekondari ya St. Peter’s Abwao iliyoko Kaunti ya Migori, ambayo hapo awali iliibuka kuwa bora zaidi mkoani humo.
Nyingine ni Mama Malia Academy katika Kaunti ya Kitui, taasisi ya kibinafsi, Shule ya Sekondari Mchanganyiko ya Kipsingei katika Kaunti ya Bomet, na Shule ya Upili ya Wavulana ya Katilu katika Kaunti ya Turkana.