logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwanaharakati Richard Otieno apatikana amefariki Molo

Otieno alishambuliwa na kuuawa na watu wasiojulikana Jumamosi usiku alipokuwa akielekea nyumbani, mita 200 tu kutoka Kituo cha Polisi cha Elburgon.

image
na Tony Mballa

Habari19 January 2025 - 14:54

Muhtasari


  • Marehemu, ambaye aliwania kiti cha Elburgon MCA mnamo 2022 na kushindwa. Alikuwa miongoni mwa wale waliokamatwa wakati wa maandamano ya Gen Z huko Molo, kwa madai ya kuongoza maandamano katika eneo hilo. 
  • Baadhi ya wakazi wa Elburgon katika Kaunti ya Nakuru mnamo Jumapili walifanya maandamano kupinga mauaji ya kiongozi wa vijana na mkosoaji wa serikali Richard Raymond Otieno na watu wasiojulikana.





Wakaazi wa mji wa Elburgon, eneo bunge la Molo kaunti ya Nakuru Jumapili walivamia kituo cha polisi cha Elburgon kufuatia mauaji ya mwanaharakati Richard Otieno.

Otieno alishambuliwa na kuuawa na watu wasiojulikana Jumamosi usiku alipokuwa akielekea nyumbani, mita 200 tu kutoka Kituo cha Polisi cha Elburgon.

Wakaazi wenye hasira waliotatiza shughuli za biashara eneo hilo Jumapili asubuhi, wanadai majibu kutoka kwa polisi.

Otieno amekuwa mkosoaji mkali wa serikali na mbunge wa eneo hilo Kimani Kuria, kwa kukosa kutimiza ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni.

Marehemu, ambaye aliwania kiti cha Elburgon MCA mnamo 2022 na kushindwa. Alikuwa miongoni mwa wale waliokamatwa wakati wa maandamano ya Gen Z huko Molo, kwa madai ya kuongoza maandamano katika eneo hilo. 

Baadhi ya wakazi wa Elburgon katika Kaunti ya Nakuru mnamo Jumapili walifanya maandamano kupinga mauaji ya kiongozi wa vijana na mkosoaji wa serikali Richard Raymond Otieno na watu wasiojulikana.

Otieno, ambaye pia anajulikana kama "Rais wa Molo", alipatikana amekufa huko Molo baada ya kuripotiwa kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa shoka.

Mwili wake uligunduliwa nje ya lango la nyumba yake ya kukodi. Washirika wa karibu wanadai kuwa aliripotiwa kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu wasiojulikana katika siku zilizopita.

Polisi walisema wanachunguza mauaji hayo. Wenyeji waliojawa na hasira walivamia chumba cha kuhifadhia maiti cha eneo hilo ambapo mwili wake ulikuwa umechukuliwa, wakauondoa na kuingia barabarani wakiandamana wakitaka haki itendeke kwa Otieno.

Polisi walitazama kwa mbali waandamanaji wakibeba mwili huo barabarani. Mbunge wa Molo Kuria Kimani aliomboleza kifo hicho na kuwataka polisi kupata undani wa kisa hicho.

“Ndugu wapiga kura, asubuhi ya leo tumeamka na taarifa za kusikitisha za kifo cha kiongozi wa vijana, mpiga kura na mhamasishaji wa jamii, Richard Raymond.

"Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinaeleza kuwa Raymond, alikumbana na kifo chake katika mazingira ya kutatanisha jana usiku (Jumamosi) na mwili wake uligunduliwa nje ya lango la nyumba yake ya kupanga," alisema.

Alisema pamoja na kwamba mazingira ya mauaji hayo bado hayajafahamika, inasadikiwa kuwa Raymond alikuwa anaelekea nyumbani ambapo watu wasiojulikana walimvamia na kumsababishia majeraha makubwa na kusababisha kifo chake.

“Nimemfahamu Raymond katika maisha yangu yote ya kisiasa na amekuwa bingwa wa kweli katika masuala yanayohusu vijana, wanawake na watu wasio na uwezo katika jamii. 

"Mchango wake kwa ustawi wa kijamii na kisiasa wa jamii inayoishi katika eneo bunge kubwa la Molo na Kaunti ya Nakuru kwa ugani, umekuwa mkubwa na umeathiri maisha ya watu wengi.” Mbunge huyo alisema.

"Kwa bahati mbaya, mkono wa kikatili wa kifo umetuibia mmoja wa wana wa kweli wa Molo ambaye ushujaa, uthabiti na ujasiri hata wakati wa taabu utawakosa wale wote ambao aligusa maisha yao kwa njia moja au nyingine".

Aliongeza kuwa amekuwa akiwasiliana na Afisa wa Uchunguzi wa Jinai wa Kanda ya Bonde la Ufa, timu za usalama za Kaunti ya Nakuru na Molo na kutaka uchunguzi wa haraka kuhusu suala hilo.

Aliwataka wakazi wa eneo hilo kuwa watulivu na kutoa muda kwa vyombo vya uchunguzi kufanya uchunguzi wao na kuwafikisha wahusika mahakamani.

Polisi walisema wanachunguza mauaji hayo.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved