Rais William Ruto amewataka viongozi wa kisiasa kuacha kuwachochea vijana wa Kenya kufanya vurugu na badala yake wawape fursa bora zaidi.
Akizungumza wakati wa ibada ya kanisa katika Kaunti ya Bungoma siku ya Jumapili, Rais Ruto alibainisha kuwa viongozi wanaochochea vijana wa Kenya kusababisha ghasia wanahusika na maendeleo duni ya nchi na badala yake wanapaswa kuwahimiza kutumia fursa zinazotolewa na serikali yake.
“Hawa vijana wa Kenya hawahitaji vurugu, hawahitaji malumbano, wanataka nafasi za kazi, na hilo ndilo tunapaswa kuwapa viongozi badala ya kuwachochea kufanya vurugu na kufanya mambo mengi ambayo hayatatatua matatizo yao,” alisema Ruto.
Ruto alisena analenga kutoa njia zaidi za kubuni nafasi za kazi na nafasi za ajira, huku akiwataka vijana kujiandikisha katika mipango ambayo tayari inapatikana.
"Kuna fursa katika uhamiaji wa wafanyikazi, vituo vya ICT, makazi, na kilimo. Kwa hivyo jipange ipasavyo na fursa hizi na maisha yako yataendelea," alibainisha.
"Msiwe na wasiwasi kuhusu wanaorusha matusi kwa sababu hawana mpango mbadala. Lakini Kenya itasonga mbele. Mnaweza kuchukua hakikisho hilo kutoka kwangu," alisema.
Haya yanajiri huku kukiwa na mvutano wa kisiasa nchini huku Ruto akizomewa na wakosoaji wake akiwemo aliyekuwa Naibu wake Rigathi Gachagua kutokana na kile wanachodai kuwa uongozi dhaifu.
Ruto ameshikilia kuwa wakosoaji wake hawatamzuia kuhakikisha kuwa miradi yake inafanikiwa.