Rais William Ruto amesema yuko sawa na jina lake la utani, "Kasongo," mradi tu nchi ifanye maendeleo.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika ziara yake ya Kanda ya Magharibi, Rais Ruto alisema kuwa Wakenya wanamtaja kama 'Kasongo' kwa sababu ni mtu mwenye busara.
“Unajua mimi ni mwerevu kuliko baadhi ya watu waliojitokeza kuniita Kasongo, na Zakayo, hilo sina tatizo ilimradi maendeleo yapo.
Wimbo maarufu "Kasongo" uliimbwa kwa mara ya kwanza mnamo 1967 na Super Mazembe, bendi ya soukous ya Kenya kutoka Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo).
Wimbo huo "Kasongo," ulioandikwa na mwimbaji mashuhuri Alley Katele, ambaye pia alianza kuimba wimbo huo, unamshirikisha mwanamke akimsihi mume wake aliyeachana naye arejee nyumbani.
Super Orchestra Mazembe ilikuwa bendi maarufu inayopiga muziki wa Soukous ambao walihama kutoka Zaire hadi Nairobi mwaka wa 1974 wakibadilisha jina lao kutoka Super Vox.
Jina lao linatafsiriwa kwa "wasogezi wa dunia kubwa. ‘Baadhi ya nyimbo maarufu za kundi hilo ni pamoja na Shauri Yako, Bwana Nipe Pesa na Samba. Kasongo alitungwa wakati wana bendi walipoenda kumtembelea rafiki yao Kasongo huko Eastleigh, Nairobi.
Walipofika nyumbani kwake, walikutana na mke wa Kasongo, na wakamuuliza kama alikuwa nyumbani.
Mke wa Kasongo aliwakaribisha na kuwaambia kwamba alikuwa hajamwona Kasongo kwa siku nyingi. Wakati huo, hakukuwa na mtandao na ilikuwa nadra kupata mtu anayemiliki simu.
Waliamua kumtumia ujumbe kwa njia ya muziki, wakitumaini kwamba ungemfikia. Wanachama wa Super Mazembe walianza kumtengenezea Kasongo wimbo sebuleni kwake, wakimwambia arudi nyumbani kwa sababu mkewe ana wasiwasi na anamtafuta lakini hampati.