SENETA wa kaunti ya Nandi ambaye pia ni kada wa kudumu wa chama cha UDA, Samson Cherargei amezua mjadala pevu kwenye mtandao wa X baada ya kutoa kauli kwamba chama hicho kitasalia madarakati kwa hadi karne moja.
Cherargei, mtetezi mkali wa sera za
serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na rais William Ruto alidai kwamba chama
cha UDA kiko imara mithili ya Simba.
Alifuatisha kauli hiyo na picha yake
akiwa amevalia sare rasmi za chama hicho – manjano, na kusema kwamba kauli
zinazoenezwa kwamba UDA kimepoteza umaarufu na uungwaji mkono nchini katika
miaka ya hivi karibuni ni kauli zisizo na ukweli wala mashiko.
Alisema UDA ni chama ambacho kimejikita vyema
katika siasa za Kenya na hicho ndicho kigezo ambacho kitakifanya kusalia
mamlakani kwa miaka 100 ijayo.
“Chama tawala kikoi mara kama
simba na wheelbarrow, na kitasalia kwenye uongozi kwa miaka 100,”
Cherargei alisema.
Kauli hii inaonekana kuwa jibu kwa
baadhi ya wanasiasa ambao katika siku za hivi karibuni wameonekana kujumuika Pamoja
kwa lengo la kuanzisha miungano mipya inayolenga kumng’oa Rais Ruto mamlakani
kupitia kura za mwaka 2027.
Wiki iliyopita, aliyekuwa naibu rais
Rigathi Gachagua alikutana na kiongozi wa chama cha NARC-Kenya Martha Karua
katika kaunti ya Kirinyaga ambapo walitangaza kuja Pamoja kwa nia moja kisiasa.
Siku mbili zilizopita, Gachagua pia
alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliojumuika katika mtaa wa Karen katika
uzinduzi wa ofisi kuu za chama cha DAP-K kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri Eugene
Wamalwa.
Hata hivyo, miungano hii haionekani
kumyumisha kivyovyote vile rais Ruto ambaye amekariri kauli kwamba wanaotaka
kushindana naye katika uchaguzi wa 2027 wana kazi nguvu sana.
Ruto alikariri kauli hiyo wiki mbili
zilizopita wakati wa ziara yake ya maendeleo ya wiki moja katika ukanda mpana
wa Magharibi mwa Kenya ambapo alisema washindani wake watakuwa na mchongoma wa
kuukwea kushindana naye.