logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Binadamu kuanza kuchimba madini Angani

Teknolojia mpya zinaongeza uwezekano wa kufanikisha uchimbaji wa madini angani.

image
na Japheth Nyongesa

Habari28 March 2025 - 09:28

Muhtasari


  • Vifaa vya ujenzi wa vyombo vya anga pia vinazidi kupatikana kwa urahisi.
  • Gharama za safari za anga zikishuka kwa kiasi kikubwa.

Minerals
Teknolojia mpya zinaongeza uwezekano wa kufanikisha uchimbaji wa madini angani.Kwa mfano, darubini ya kisasa ya Vera C. Rubin nchini Chile, ambayo iko karibu kukamilika, itasaidia kutambua na kufuatilia miamba ya angani kwa urahisi zaidi.

Vifaa vya ujenzi wa vyombo vya anga pia vinazidi kupatikana kwa urahisi, huku gharama za safari za anga zikishuka kwa kiasi kikubwa.

Miaka 15 iliyopita, iligharimu takriban dola 10,000 kupeleka mzigo wa kilo 0.45 angani. Lakini sasa, gharama hiyo imeshuka hadi chini ya dola 2,000, na kwa teknolojia mpya kama SpaceX Starship, kuna matumaini kuwa gharama inaweza kushuka hadi mamia ya dola tu.

Kupungua kwa gharama za safari za anga ni mojawapo ya sababu zinazoharakisha ndoto ya uchimbaji wa miamba ya angani.

 Neil deGrasse Tyson, aliwahi kusema kuwa bilionea wa kwanza wa trilioni atatokana na uchimbaji wa madini angani. Hii ni kwa sababu miamba ya angani ina utajiri mkubwa wa madini adimu kama platinamu, nikeli, kobalti, na hata helium-3, ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia.

Wataalamu wengine wanahoji kuwa uchimbaji huu unaweza kusaidia kuhifadhi mazingira ya Dunia kwa kupunguza utegemezi wa madini ya ardhini, ambayo uchimbaji wake unasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira. Kwa mfano, uchimbaji wa platinamu ardhini unahitaji nishati kubwa na hutoa kiasi kikubwa cha gesi chafu.

Kulingana na utafiti wa mwaka 2018 wa Chuo Kikuu cha Paris-Saclay, uchimbaji wa platinamu kwenye miamba ya angani ungetoa kilo 150 za hewa chafu kwa kila kilo moja ya platinamu inayopatikana.

Kwa kulinganisha, uchimbaji wa madini hayo duniani hutoa hadi kilo 40,000 za hewa chafu kwa kiasi hicho hicho cha platinamu. Kwa mujibu wa Daynan Crull, mwanzilishi wa kampuni ya Karmen+, uchimbaji wa madini angani unaweza kuchochea uchumi wa anga, ambao Kituo cha Kiuchumi Duniani (WEF) kinatabiri kufikia thamani ya dola trilioni 1.8 ifikapo mwaka 2035.

Licha ya matumaini makubwa, wapo wanaohoji uhalisia wa uchimbaji wa madini angani. Profesa Lang, mtaalamu wa masuala ya madini, anasema kuwa ingawa kiteknolojia inawezekana, gharama kubwa za mradi huu zinaweza kufanya biashara hii isiwe na faida.

Anaeleza kuwa madini kama platinamu bado yanapatikana ardhini, hata kama yapo chini ya bahari, na teknolojia mpya zinaweza kuwezesha uchimbaji wake kwa urahisi zaidi kuliko kutumia mabilioni ya dola kusafiri angani.

Mtaalamu wa mazingira Kathryn Miller, kutoka Chuo Kikuu cha Lancaster, anaamini kuwa uchimbaji wa madini angani ni bora zaidi kwa mazingira kuliko uchimbaji wa kina kirefu cha baharini.

Anasema kuwa kuchimba madini kwenye sakafu ya bahari kunasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ya baharini, ikiwemo kuteketeza viumbe wa baharini na mifumo yao ya ikolojia.

Hata hivyo, uchimbaji wa miamba ya angani pia unakabiliwa na changamoto za kimazingira. Wanamazingira wana wasiwasi kuwa mabaki na vumbi litakavyotokana na uchimbaji angani vinaweza kuzidisha tatizo la uchafuzi wa anga. Pia, kuna hofu kwamba vipande vya miamba vilivyopasuka vinaweza kuanguka na kuingia tena kwenye anga ya Dunia.

"Anga za juu zinapaswa kubaki safi. Tunapaswa kuhakikisha tunasafisha baada ya shughuli zetu angani," anasema Dkt. Monica Grady, mhadhiri wa sayansi ya anga na sayari katika Chuo Kikuu Huria cha Uingereza.

Hata hivyo, wawakilishi wa sekta hii wanapinga hoja hiyo, wakisema kuwa rasilimali za anga zinapaswa kutumiwa kwa manufaa ya wanadamu. "Anga ina rasilimali zisizo na mwisho, lakini Dunia yetu ni moja tu. Lazima tutafute njia za kuhifadhi rasilimali za Dunia kwa manufaa ya vizazi vijavyo," alisema mmoja wa wakurugenzi wa AstroForge.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved