
Rigathi Gachagua, mwenyekiti wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), amelaani matumizi ya nguvu kupita kiasi ya serikali dhidi ya waandamanaji wa kizazi cha Gen Z waliokuwa wakifanya maandamano kwa amani.
Gachagua alihusisha ghasia zilizoshuhudiwa wakati wa maandamano hayo na utawala wa Rais William Ruto.
“Chanzo cha maandamano ya Gen Z kinajulikana vizuri na Serikali pamoja na kila Mkenya; Bwana Ruto, unajua uliwaahidi vijana wetu ajira na ukombozi wa kiuchumi. Unajua ulichowapatia wao pamoja na wazazi wao,” alisema.
“Kuwatisha waandamanaji wa amani na vijana waliokuwa wakikumbuka wenzao waliouawa katika mapambano haya, kunaifanya hali kuwa ngumu zaidi kwa wewe na utawala wako dhalimu, Bwana Ruto,” aliongeza.
Aliikosoa polisi kwa kutumia risasi za moto na nguvu kupita kiasi dhidi ya vijana waliokuwa wakiandamana kwa amani kuwakumbuka wenzao waliopoteza maisha.
“Kwa maneno makali kabisa, nalani matumizi ya nguvu kupita kiasi na risasi za moto na polisi dhidi ya waandamanaji wa Gen Z waliokuwa wa amani na wasiokuwa na hatia, kama ilivyoshuhudiwa jana kote nchini,” alisema Gachagua.
Gachagua alimlaumu Rais Ruto kwa kushindwa kutekeleza ahadi za kuunda ajira na kuwawezesha vijana kiuchumi, jambo alilolitaja kuwa ndio kiini cha maandamano hayo.
Mwenyekiti huyo wa DCP alimshtumu Rais Ruto na Gavana wa Nairobi kwa kupanga ghasia wakati wa maandamano, ikiwa ni pamoja na kutumia wahuni kuwatisha na kuwashambulia waandamanaji wa amani badala ya kushughulikia malalamiko yao.
“Tuna habari za kuaminika kwamba jijini Nairobi, hasa katika eneo la katikati ya jiji, biashara za watu kutoka jamii fulani zilitambuliwa wazi na maafisa wa serikali ya kaunti ya Nairobi na maeneo mengine, shughuli hii ya kikatili iliongozwa na wanasiasa walioko upande wa utawala huu dhalimu.”
“Kwa kushirikiana na polisi, maafisa na wanasiasa hawa waliongoza wahuni kuvamia maeneo maalum kwa ajili ya uporaji kwa lengo la kuwatisha na kuwalazimisha watu kuunga mkono utawala huu usiokubalika. Tunafahamu kuwa biashara nyingi ziliachwa salama jioni, lakini asubuhi zilipatikana tayari zimeporwa,” alisema.
“Bwana Ruto, unajua vyema kwamba kwa maagizo yako, waandamanaji halisi wa Gen Z walizuiwa kwa maelfu katika barabara ya Kiambu na Thika ambapo hakuna biashara zilizoporwa.”
“Polisi wako waliwaruhusu wahuni kuingia jijini kwa gharama ya walipa kodi ili kuleta vurugu na kuwalaumu Gen Z.”
Kumekuwa na madai kuwa biashara zinazomilikiwa na baadhi ya jamii zilikusudiwa kushambuliwa wakati wa uporaji ulioratibiwa na washirika wa serikali kwa nia ya kueneza hofu na kupata uungwaji mkono kwa utawala uliopo.
Gachagua alionyesha mshangao kwamba serikali ilizima matangazo ya vituo vikuu vya runinga wakati wa machafuko hayo ili kuwezesha uporaji uliopangwa chini ya ulinzi wa polisi.
“Serikali ilizima makusudi matangazo ya vituo vikuu vya runinga nchini katika mpango uliopangwa wa kuhakikisha kuwa wahuni waliodhaminiwa na serikali wanapora na kuharibu mali chini ya ulinzi wa polisi,” alisema.
Alipinga vikali madai ya msemaji wa serikali aliyedai kuwa maandamano ya Gen Z ni ya kikabila, akisisitiza kuwa vijana hao wameungana dhidi ya ufisadi na ghasia.
Gachagua alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kusikilizwa kwa kuwa wao ni mustakabali wa Kenya na wamekuwa wakibaguliwa na kunyanyaswa mara kwa mara na dola.
Alitangaza kufutilia mbali mkutano wake na wanahabari pamoja na shughuli nyingine za umma ili kuwaenzi waathiriwa wa maandamano na kusimama pamoja na walioathiriwa na hatua za serikali.