
Vipande vya risasi vilivyopasua fuvu la kichwa cha Boniface Kariuki baada ya kupigwa risasi kwa karibu bado vimejikita ndani kabisa ya ubongo wake, na kuongeza hali ambayo madaktari wameitaja kuwa ya hatari sana na inayohitaji uangalizi wa hali ya juu katika safari ya kupona.
Madaktari walimtangaza kuwa hana fahamu (brain dead) siku ya Jumapili. Kwa mujibu wa familia yake, timu ya matibabu katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) tayari imefanya upasuaji mkubwa mara tatu, lakini imeonya kuwa kuondoa vipande vilivyobaki vya risasi kunaweza kuhatarisha maisha yake.
Kariuki, mwenye umri wa miaka 22, ameendelea kuwa katika hali mahututi KNH kwa wiki mbili sasa, tangu tarehe 17 Juni alipopigwa risasi kichwani kwa karibu na afisa wa polisi wakati wa maandamano ya kumtaka Naibu Inspekta Jenerali Eliud Lagat ajiuzulu. Alikimbizwa hospitalini kwa matibabu ya dharura.
Wakati wa upasuaji wa kwanza, madaktari waliweza kuondoa risasi kuu, lakini vipande kadhaa vya chuma bado vimebaki kwenye ubongo wake. Kwa mujibu wa madaktari, vipande hivyo vipo katika maeneo ambayo ni hatari sana kufanyiwa upasuaji bila kuhatarisha maisha yake.
Ijumaa, Kariuki alifanyiwa upasuaji wa tatu kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuimarisha hali yake.
Msemaji wa familia, Emily Wanjiru, alisema upasuaji wa hivi karibuni ulilenga kuhamisha mirija ya kupumua kutoka puani hadi kwenye koo ili kumwezesha kupumua kwa kutumia oksijeni ya kawaida.
“Sehemu ya upasuaji huo ilihusisha hatua iitwayo pegging, ambayo huunda njia ya kupitishia mirija ya chakula chini ya tumbo, ikielekezwa kwa utumbo kwa wagonjwa wasioweza kumeza,” Wanjiru aliambia The Standard.
Alieleza kuwa njia hiyo haihusishi upasuaji mkubwa wa tumbo na husaidia kuwapatia wagonjwa mahututi lishe muhimu kwa njia salama.
Kwa mujibu wa Wanjiru, madaktari walisema kuna kipande kimoja cha risasi kilichosalia kwenye ubongo ambacho hakiwezi kuondolewa kwa sasa.
“Walisema kitaondolewa tu pale kitakapotoa usaha. Wana hofu kuwa kukigusa sasa kunaweza kuhatarisha maisha yake,” alisema.
Wanjiru pia alifichua kuwa ubongo wa Kariuki umeharibika vibaya.
“Hamwajui mtu yeyote, lakini Jumatatu alikuwa akijibu kwa maumivu kabla ya kurudi katika hali ile ile ya awali,” alisema.
Kutokana na hali yake, Kariuki atalazimika kubaki katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa muda usiojulikana.
Wakati huo huo, familia inakabiliwa na mzigo mkubwa wa gharama ya hospitali ambayo inaripotiwa kuvuka Shilingi milioni 2.7.
“Kwa siku moja, tuliambiwa bili huongezeka kwa Shilingi 180,000. Hali hiyo imetulazimu kufungua nambari ya mchango kwa sababu wazazi wake hawawezi kuimudu,” Wanjiru aliongeza.