Maafisa wa Kikosi cha Ulinzi cha Kenya (KDF) watalazimika kuchangia kwa kiasi kikubwa kugharamia milo yao kuanzia Julai 1, kufuatia uamuzi wa serikali wa kuondoa ruzuku ya chakula cha mchana iliyokuwa ikilipiwa na hazina ya serikali.
Wizara ya Ulinzi (MOD) imeanzisha mfumo mpya wa “Lipa Kadri Unavyokula” (Pay-As-You-Eat - PAYE) kuchukua nafasi ya mpango wa awali wa chakula cha mchana kilichopunguzwa bei.
Hatua hii imeibua wasiwasi, hasa miongoni mwa maafisa wa ngazi ya chini ambao kwa muda mrefu wametegemea milo hiyo ya ruzuku katika hali ngumu ya kiuchumi.
Kulingana na wizara, sera hii mpya inalenga kurahisisha mgao wa bajeti na kuboresha ufanisi wa matumizi ya rasilimali za serikali.
Maafisa wa serikali wanasema kuwa uamuzi huo umetokana na haja ya kisasaisha taratibu za utendaji jeshini kama sehemu ya mageuzi mapana katika sekta ya umma.
Aidha, wizara imefafanua kuwa mabadiliko haya hayajalenga kuondoa manufaa ambayo maafisa walikuwa wakifurahia hapo awali, bali yamelenga kuendana na viwango bora vya kimataifa vya kijeshi.
Imesisitiza kuwa lengo ni kutoa unafuu na urahisi kwa wanajeshi na kuboresha ufanisi wa gharama kwa ujumla.
“Uamuzi wa kuhamia kutoka mfumo wa chakula cha mchana kilicholipiwa na serikali hadi mfumo wa Pay-As-You-Eat umetokana na hitaji la kurahisisha mgao wa bajeti, kuboresha matumizi ya rasilimali za serikali, kurahisisha upatikanaji wa aina mbalimbali za milo kulingana na mapendeleo ya mtu binafsi, na kuendana na viwango bora vya kijeshi katika ukanda huu na kimataifa,” wizara ilisema.
“Mpango wa chakula cha mchana uliokuwa ukilipiwa na serikali umeonekana kutokuwa wa gharama nafuu. Haukuwapa wanajeshi uhuru wa muda wala urahisi wa mahali pa kula, na umelaumiwa kwa kupoteza saa za kazi kutokana na misururu mirefu pamoja na marudio ya mgao wa chakula wakati wanajeshi wanapohamishwa kambi,” taarifa hiyo iliongeza.
Tayari, Makao Makuu ya Jeshi la Nchi Kavu yamepitisha waraka kwa kambi zote na vituo vya operesheni kuhusu mabadiliko hayo ya mfumo wa malipo, ambao utaanza kutekelezwa kesho.
Waraka huo umeagiza kambi kujiandaa ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa miundombinu ya migahawa, vifaa na huduma vinavyohitajika viko tayari kuunga mkono mpango wa Pay-As-You-Eat.
Aidha, imeelezwa kuwa mahitaji ya ziada yatashughulikiwa hatua kwa hatua kulingana na mazingira ya kila kambi katika mwaka wa fedha wa 2025/2026.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, serikali imeongeza juhudi za kudhibiti matumizi ya umma kama sehemu ya mageuzi ya kifedha yanayolenga kupunguza nakisi ya bajeti ya kitaifa na kudhibiti ongezeko la deni la taifa.
Hazina ya Kitaifa imekuwa ikitekeleza sera za kupunguza matumizi, ikiwa ni pamoja na kupunguza bajeti katika wizara, idara za serikali na mashirika ya umma.
Hatua hizi zimejumuisha kusitisha miradi mipya, kuunganisha taasisi zinazofanya kazi zinazofanana, pamoja na kupunguza safari zisizo za lazima na posho.
Hatua hizo pia zimehusisha utekelezaji wa bajeti kulingana na utendaji na mabadiliko ya kuelekea kugawana gharama katika shughuli zisizo za msingi za serikali, kama vile ruzuku ya chakula mashuleni, bima ya afya, na vifaa vya kijeshi.
Kuondolewa kwa ruzuku ya chakula cha mchana kwa KDF ni sehemu ya juhudi za serikali kupunguza matumizi ya kawaida na kuelekeza fedha kwenye vipaumbele vya maendeleo.