
Mswada mpya uliodhaminiwa na Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Nairobi, Esther Passaris, unalenga kupiga marufuku mikutano ya umma karibu na majengo ya Bunge na maeneo yote yaliyo chini ya ulinzi maalum.
Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Utaratibu wa Umma wa mwaka 2025 unapendekeza mabadiliko katika Sheria ya Utaratibu wa Umma (Sura ya 56) ili kushughulikia mikutano ya hadhara na maandamano, kwa kuweka mipaka ya maeneo ya mikusanyiko na maandamano.
Mbunge huyo wa kaunti anasisitiza kuwa mikutano au maandamano yoyote ya umma hayapaswi kufanyika ndani ya mzunguko wa mita 100 kutoka maeneo ya Bunge, maeneo ya kulindwa chini ya Sheria ya Maeneo Yaliyolindwa, na mahakama.
“Yeyote atakayekiuka masharti ya sehemu hii atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atatozwa faini isiyozidi shilingi laki moja au atahukumiwa kifungo kisichozidi miezi mitatu, au adhabu zote mbili,” sehemu ya mapendekezo hayo inasomeka.
Mswada huo pia unampa Waziri wa Usalama wa Ndani mamlaka ya kuainisha maeneo ya mikutano na maandamano kwa kushauriana na serikali za kaunti, na kuainisha maeneo ambayo mikutano ya umma na maandamano hayaruhusiwi.
Sura ya 56 ya Sheria ya Utaratibu wa Umma inadhibiti mikutano ya hadhara na maandamano, ikitaka taarifa kutolewa kwa afisa wa polisi angalau siku tatu kabla ya tukio.
Sheria hiyo inaeleza taratibu za kuandaa mikusanyiko ya umma, ikiwa ni pamoja na sharti kwa waandaaji kutoa taarifa zenye maelezo kama majina, anwani, tarehe, muda (kati ya saa 12 asubuhi na saa 12 jioni), na mahali pa mkutano.
Sheria hiyo pia inashughulikia mikusanyiko isiyo halali na athari kwa wanaohusika. Wale watakaohusika wanaweza kushtakiwa chini ya vifungu vya Kanuni ya Adhabu kuhusu mikusanyiko haramu na kuhukumiwa kifungo.