Aliyekuwa Seneta Mteule Gloria Orwoba ameagizwa na Mahakama ya Biashara ya Milimani kumlipa Karani wa Seneti Jeremiah Nyegenye fidia ya KSh10.5 milioni.
Haya yanajiri baada ya mbunge huyo kupatikana na hatia ya kumdhalilisha Nyegenye kwa kuchapisha ujumbe wa chuki na uongo kwenye mitandao ya kijamii, akimshutumu kwa unyanyasaji wa kimapenzi
Katika uamuzi uliotolewa Jumatatu, Julai 14, Hakimu Ruguru Ngotho alisema kwamba kauli za Orwoba zilizochapishwa kwenye hali ya WhatsApp, ukurasa wake wa Facebook na mtandao wa X zilikuwa za uongo, za kashfa, na zenye nia mbaya.
Aidha, mahakama ilibaini kuwa madai hayo ya unyanyasaji wa kimapenzi hayakulindwa na kinga ya kibunge na yalitolewa kwa nia ovu.
“Maneno yaliyowekwa na kuchapishwa na Mshitakiwa kumhusu Mlalamikaji ni ya kashfa, ya kuchafua jina, na yenye nia ya kumharibia,” alisema hakimu.
Kwa msingi huo, mahakama ilimpatia Nyegenye fidia ya jumla ya KSh8 milioni na KSh2.5 milioni kama fidia ya adhabu na mateso yaliyoongezwa.
Zaidi ya hayo, Nyegenye atapata fidia ya KSh1 milioni endapo Orwoba hatatoa msamaha wa hadharani ndani ya siku 30 kupitia mitandao yake ya kijamii na katika gazeti la kitaifa.
Mahakama pia ilitoa agizo la kudumu linalomzuia Orwoba au washirika wake kuchapisha taarifa zozote za kashfa dhidi ya Karani huyo wa Seneti.
Orwoba alimshtumu Nyegenye kwa kumbembeleza kimapenzi na kulipiza kisasi baada ya kukataa.
Katika video aliyoweka kwenye Facebook na ambayo ilitumiwa kama ushahidi mahakamani, Orwoba alisema, “Karani wa Seneti Jeremiah Nyegenye aliniomba msaada wa kimapenzi... na nilipokataa... kulianza kulipiza kisasi.”
Hata hivyo, mahakama ilisema kwamba Orwoba hakutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.
“Ilipaswa awe amejitahidi zaidi kuthibitisha kauli zake. Hakufanya hivyo,” alisema hakimu.
Uamuzi huo ulieleza kuwa ujumbe wa Orwoba ulikuwa na nia ya kuharibu taaluma na sifa ya Nyegenye, si kutafuta haki.
“Lengo lake kuu lilikuwa kumuondoa Karani wa Seneti kwa kumchafua na kumdhalilisha,” ilisema mahakama.
Mahakama pia ilielezea kutoridhishwa na mienendo ya Orwoba katika kesi hiyo, ikisema hakuonyesha ushirikiano wala majuto.
“Mienendo ya Mshitakiwa imekuwa ya mzaha. Fidia ya adhabu inafaa ili kumkumbusha kuwa uhuru wa kujieleza unapaswa kutumiwa kwa uwajibikaji,” iliongeza mahakama.
Kwa upande wake, Nyegenye ambaye aliwakilishwa na wakili Peter Wanyama, alieleza kuwa madai hayo yalileta madhara makubwa kwa familia yake na maisha yake ya kikazi.
Shahidi mwingine ambaye ni mfanyakazi mwenzake pia alithibitisha kuwa madai hayo hayakuwa ya kweli na yalimchafua sana katika jamii na taaluma yake.
Hata hivyo, Orwoba alikiri kuchapisha taarifa hizo na kusema aliamini zilikuwa za kweli, lakini mahakama ilisema kuwa hoja zake za kujitetea hazikuwa na msingi wa kisheria.
“Hakuna kiasi cha pesa kinachoweza kurejesha heshima ya mtu iliyoharibiwa. Mahakama hii inaweza tu kujaribu kupoza madhara ya sifa ya Mlalamikaji,” alisema Hakimu Ruguru Ngotho.