Atwoli afichua mazungumzo yake na Raila kabla ya kukutana na Rais Ruto

Alisema hatua yake ilichochewa na kazi yake ya kuwawakilisha wafanyikazi.

Muhtasari

• Atwoli amefichua kuwa alizungumza na kiongozi wa ODM Raila Odinga kabla ya mkutano wake na Rais William Ruto katika Ikulu siku chache zilizopita.

•Pia alisisitiza kuwa atashirikiana na serikali  kwa manufaa ya Wakenya.

Katibu wa COTU Francis Atwoli akutana na rais William Ruto.
Katibu wa COTU Francis Atwoli akutana na rais William Ruto.
Image: HISANI

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli amefichua kuwa alizungumza na kiongozi wa ODM Raila Odinga kabla ya mkutano wake na Rais William Ruto katika Ikulu siku chache zilizopita.

Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika Khwisero katika kaunti ya Kakamega siku ya Jumamosi, Atwoli alifichua kwamba alimwambia Raila kuwa hatua yake ilichochewa na kazi yake ya kuwawakilisha wafanyikazi Wakenya.

“Nilimweleza Raila kuwa nina eneo langu ninalowakilisha na ninajihusisha na siasa za uwakilishi ambapo ninaunga mkono masuala yanayohusiana na wafanyakazi, lakini hatukupata urais,” alisema.

“Kama kiongozi wa kimataifa wa wafanyikazi, nilienda kwa wale walioipata (uongozi) ili wanisaidie kutekeleza viwango vya mkataba wa kimataifa wa wafanyikazi,"

Aidha, Atwoli alifichua kuwa alikutana na Rais William Ruto ili kujadili masuala muhimu ya kitaifa  yanayohusu Wakenya.

Alisema kiongozi huyo wa taifa anataka upinzani kuendelea kutoa shinikizo kwa serikali, haswa kuhusu masuala muhimu yanayowahusu Wakenya.

"Rais Ruto anakubaliuUpinzani lazima uwe na nguvu na uendelee kufanya kile kinachostahili kufanya," alisema.

Alibainisha kuwa walijadili zaidi kuhusu nafasi za ajira hatari zinazoinyima serikali nafasi ya kukusanya kodi.

"Serikali haipati kodi kutoka kwa wafanyikazi wa nje. Watumishi hao hawalipi NSSF wala NHIF. Hayo ni mazungumzo tuliyofanya na Rais,” alisema.

Pia alisisitiza kuwa atashirikiana na serikali  kwa manufaa ya Wakenya.

Mnamo Alhamisi, Atwoli alikutana na Rais  Ruto, siku chache baada ya kudokeza  kufanya kazi na serikali ya Kenya Kwanza.

Alikuwa katika kambi ya Raila Odinga ya Azimio la Umoja wakati wa kampeni za kabla ya  uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Aliendesha kampeni kali dhidi ya urais wa Ruto, na wakati fulani alirekodiwa akisema kuwa Ruto kamwe hatamrithi Rais wa zamani Uhuru Kenyatta.

Atwoli alikuwa sehemu ya wajumbe kutoka jamii ya Waluhya waliokutana na Ruto Ikulu Alhamisi.

Wengine walioandamana naye ni katibu mkuu wa baraza la mawaziri Musalia Mudavadi, Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale, aliyekuwa mgombeaji wa ugavana wa Kakamega Cleophas Malala na Rashid Echesa, miongoni mwa wengine.