UDA yashinda kinyang'anyiro cha Kiambaa

John Njuguna Wanjiku ni mbunge wa kwanza kuchaguliwa kwa tikiti ya chama cha UDA ambacho kinajihusisha na naibu rais William Ruto

Muhtasari

• Shughuli ya kuhesabu kura ilikuwa imesitishwa kwa muda baada ya mgombea kiti na tikiti ya Jubilee Kariri Njama pamoja na wafuasi wake kudai kuwepo kwa ulaghai katika shughuli hiyo

Image: HISANI

Hatimaye shughuli ya uhesabu wa kura katika eneo bunge la  Kiambaa imekamilika huku mgombea kiti na chama cha UDA akiibuka mshindi.

Njuguna ameibuka mshindi baada ya kuzoa kura 21,773 akifuatwa kwa karibu na Kariri Njama wa Jubilee aliyepata kura 21,263.

Ingawa IEBC haijatangaza rasmi ushindi wa Njuguna, kura za vituo vyote `154 zimeweza kujumuishwa.

Shughuli ya kuhesabu kura ilikuwa imesitishwa kwa muda baada ya mgombea kiti na tikiti ya Jubilee Kariri Njama pamoja na wafuasi wake kudai kuwepo kwa ulaghai katika shughuli hiyo.

Kaariri Njama akiungwa mkono na wafuasi wake walikabiliana na maafisa wa usalama wakiagiza kuhesabiwa tena kwa kura za vituo vitatu.

Mwanasiasa huyo na wafuasi wake hawakuridhishwa na matokeo ambayo yalitangazwa kutoka vituo vya Cianda, Gachie na Muchatha. Walidai kuwa matokeo yalikuwa yamebadilishwa kwa mapendeleo mgombea kiti na tikiti ya UDA John Njuguna.

Hata hivyo, Njuguna amemshawishi mwenzake wa Jubilee kukubali matokeo akisema kuwa kwa kila kinyang'anyiro lazima kuwe na mshindi na atakayeshindwa.

Katibu mkuu wa chama cha UDA Veronica Maina amepongeza IEBC kwa kuweza kuendeleza uchaguzi huo kwa utaalamu na kwa kuweza kusuluhisha mgogoro uliokuwepo kuhusiana na uhesabu wa kura.

Wadadisi wengi wa maswala ya kisiasa wamesema kuwa chaguzi hizo ndogo ambazo zilifanyika katika ngome ya rais Uhuru Kenyatta zitabaini umaarufu wa rais dhidi ya naibu wake William Ruto ambaye anaegemea upande chama cha UDA.