Nick Mwendwa atiwa mbaroni tena baada ya faili ya kesi yake kufungwa

Muhtasari
  • Ripoti hizo zilithibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa FKF Barry Otieno mnamo Ijumaa
  •  Mwendwa anazuiliwa katika Makao Makuu ya DCI kando ya Barabara ya Kiambu
  • Mnamo Alhamisi, upande wa mashtaka uliambia mahakama kwamba ungependa kuifunga kesi hiyo kwa sasa
Image: MAKTABA

Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa amekamatwa tena.

Ripoti hizo zilithibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa FKF Barry Otieno mnamo Ijumaa.

 Mwendwa anazuiliwa katika Makao Makuu ya DCI kando ya Barabara ya Kiambu.

Mnamo Alhamisi, upande wa mashtaka uliambia mahakama kwamba ungependa kuifunga kesi hiyo kwa sasa.

DPP alikuwa amepatiwa siku saba kupendekeza mashtaka dhidi ya Mwendwa lakini amechagua kufunga faili yake.

"Tunataka kufunga faili yetu huku timu yetu ikiendelea na uchunguzi wa kesi hiyo kwa kasi yetu kabla ya kupendekeza mashtaka dhidi yake," alisema DPP.

Hakimu mfawidhi wa mahakama ya Milimani Wandia Nyamu aliruhusu ombi la DPP na kuamuru kesi hiyo kufungwa.

Siku ya Alhamisi DPP na DCI walitarajiwa kufahamisha mahakama iwapo walikuwa wamekamilisha uchunguzi dhidi ya Mwendwa na kupendekeza mashtaka yafaayo.