Sonko na familia yake wapigwa marufuku kuingia Marekani

Familia ya Sonko ilipigwa marufuku kutokana na biashara za ufisadi. Hata hivyo, amekanusha mashtaka haya yote

Muhtasari

• Familia yake inajumuisha Mke Primrose, binti - Saumu na Salma, na mtoto wake mdogo. Zote haziruhusiwi kuingia Marekani.

• "Marekani ina habari za kuaminika kwamba Sonko alihusika katika ufisadi alipokuwa gavana wa Nairobi," idara hiyo ilisema Jumanne.

Mike Sonko
Image: EZEKIEL AMING'A

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amepigwa marufuku kuingia Marekani kwa madai ya ufisadi ‘mkubwa’ alipokuwa Gavana. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken alisema Sonko na familia yake hawana sifa ya kuingia nchini kuanzia sasa. Familia yake inajumuisha mkewe Primrose, mabinti - Saumu na Salma, na mtoto wake mdogo. Wote hawaruhusiwi kuingia Marekani.

 "Marekani ina habari za kuaminika kwamba Sonko alihusika katika ufisadi alipokuwa gavana wa Nairobi," idara hiyo ilisema Jumanne.

 "Kwa hili, idara inathibitisha hitaji la uwajibikaji na uwazi nchini Kenya," alisema Eric Watnik, Mshauri wa Diplomasia ya umma katika ubalozi wa Marekani mjini Nairobi.

 Idara hiyo ilisema shughuli za ufisadi zilitokana na zabuni na utoaji wa kandarasi kinyume na utaratibu kwa manufaa yake binafsi. Sonko alishtakiwa mnamo Desemba 4, 2020 katika kile wengi walifananisha matukio ya filamu ya kulala tajiri na kuamka maskini.

 Gavana huyo wa zamani wa mji mkuu wa Kenya, Nairobi, sasa anakabiliwa na mashtaka mbali mbali ya uhalifu ikiwa ni pamoja na kesi kadhaa za ufisadi, shambulio na makosa yanayohusiana na ugaidi. Sonko amekanusha madai na mashtaka yote.

Anadaiwa kufuja zaidi ya shilingi milioni 300 kwa njia ya utoaji wa kandarasi zisizo za kawaida kwa kampuni za marafiki ambazo zinasemekana kuwa na pesa kwenye akaunti zake za kibinafsi baada ya kupokea malipo yao kutoka kaunti ya Nairobi.

 Hivi majuzi pia alishutumiwa kwa kusajili na kuwapa silaha wanamgambo, kununua nguo za kijeshi zinazohusiana na vikundi vya kigaidi na kufadhili shughuli za kigaidi. 

Mnamo Februari 24, Sonko alipoteza ombi lake la kusimamisha mashtaka yake katika kesi ya ufujaji wa shilingi milioni 357 inayoendelea katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi huko Milimani.

Kuna uwewezekano finyu kwa Sonko kubatilisha marufuku hiyo.Idara hiyo ilisema huu ni uamuzi uliofanywa nje ya mamlaka ya mahakama."Sijui ana njia zipi kisheria, uamuzi huo unatokana na sheria ya uhamiaji,” alisema Watnik. 

Kulingana na Marekani, suala la Sonko halichochewi kisiasa.

"Hili ni suala la uhamiaji kwa Amerika. Ni kuhusu Marekani na jinsi inavyoathiri maslahi ya Marekani na nje. Tunaangazia madhara yaliyofanywa nchini Kenya na demokrasia yake. Uamuzi huo ulifanywa kwa kuzingatia ni nani tunafikiri haruhusiwi kusafiri hadi Marekani,” Watnik alisema.

Idara hiyo ilisema Sonko hajui kuhusu mashtaka yatakayomkabili lakini ikabainisha kuwa pindi tu atakapopokea mawasiliano hayo, anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.