COVID 19: Amri ya kuvaa barakoa yaondolewa

Muhtasari

•Karantini ya lazima pia imeondolewa kwa watu waliochanjwa na wale ambao bado hawajapokea chanjo.

•Kagwe amewahimiza wale ambao hawajachanjwa bado kupiga hatua hiyo ili kulinda familia zao.

Waziri wa Afya Mutai Kagwe wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu Covid-19 katika nyumba ya afya mnamo Machi 11, 2022.
Waziri wa Afya Mutai Kagwe wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu Covid-19 katika nyumba ya afya mnamo Machi 11, 2022.
Image: MERCY MUMO

Waziri wa afya Mutahi Kagwe ametangaza kuondolewa kwa amri ya kuvaa Barakoa.

Akizungumza katika Afya House siku ya Ijumma, Kagwe amesema Wakenya wako huru kutoka nje bila barakoa.

Maeneo ya ibada na magari ya umma pia yameruhusiwa kubeba idadi kamili ya watu.

Kagwe hata hivyo amewaagiza Wakenya kuendelea kuvaa barakoa katika hafla za ndani na wanaposafiri kutumia magari ya umma.

Wakenya pia wamehimizwa kuzingatiza mikakati mingine ya kuzuia maambukizi ya Corona kama vile kunawa mikono mara kwa mara na kuepuka maeneo yenye watu wengi.

Karantini ya lazima pia imeondolewa kwa watu waliochanjwa na wale ambao bado hawajapokea chanjo.

Michezoni, waziri ameruhusu viwanja vyote kubeba idadi kamili ya mashabiki. Mashabiki wote wataruhusiwa viwanjani mradi tu wamechanjwa.

Waziri wa afya ameweka wazi kwamba serikali haitawashurutisha Wakenya kupoka chanjo.

Hata hivyo, Kagwe amewahimiza wale ambao hawajachanjwa bado kupiga hatua hiyo ili kulinda familia zao.

“Kuchanjwa ni hatua ya kujitolea.Hakuna atakayeshurutishwa kupokea chanjo. Serikali ina chanjo tosha,“ Kagwe amesema.

Kagwe amesema kuwa mikakati mipya huenda ikarejelewa wakati wowote.