Mike Sonko kuwania ugavana Mombasa

Muhtasari

•Jina la Sonko lipo kwenye orodha ya wanasiasa sita ambayo Wiper ilipitisha kwa IEBC kama wagombeaji walioidhinishwa kuwania nyadhfa za kisiasa katika kaunti mbalimbali.

•Mtihani mkubwa zaidi unasalia ikiwa IEBC itamuidhinisha Sonko kuwania kiti hicho ikizingatiwa kuwa bado kuna kesi zinazomkabili mahakamani.

Mwanasiasa na mfanyibiashara mashuhuri nchini Mike Sonko anazamia kurithi Hassan Joho kama gavana wa pili wa Mombasa.

Sonko atawania ugavana wa kaunti hiyo ya Pwani kwa tikiti ya Wiper.

Jina la Sonko lipo kwenye orodha ya wanasiasa sita ambayo Wiper ilipitisha kwa IEBC kama wagombeaji walioidhinishwa kuwania nyadhfa za kisiasa katika kaunti mbalimbali.

Haya yanajiri wiki chache tu baada yake kugura chama tawala cha Jubilee na kujiunga na Wiper inayoongozwa na Kalonzo Musyoka.

Akizungumza katika kituo kimoja cha redio, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya Wiper Agatha Solitei alithibitisha kuwa Sonko atachuana na Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo kwenye kura za mchujo.

"Hiyo ndiyo orodha ambayo tumetuma kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, na ndiyo Sonko amejiwasilisha kama mgombeaji katika kinyang'anyiro cha Ugavana wa Mombasa," alisema.

Mtihani mkubwa zaidi unasalia ikiwa IEBC itamuidhinisha Sonko kuwania kiti hicho ikizingatiwa kuwa bado kuna kesi zinazomkabili mahakamani.

Sonko alivuliwa mamlaka kama gavana wa Nairobi mnamo Desemba 2, 2020 ambapo wajumbe 88 wa Nairobi walipiga kura kumbandua. Mnamo Desemba 17, 2020 Seneti ilishikilia uamuzi wa bunge la kaunti ya Nairobi kumng'atua gavana wao mamlakani.