Mwanariadha wa kike apatikana ameuawa Iten

Crime Scene

Mwanariadha wa kike amepatikana ameuawa katika nyumba moja katika mji wa Iten.

Mwanariadha huyo chipukizi ametambuliwa kama Damaris Muthee Mutua mwenye umri wa miaka 24.

Inadaiwa aliuawa na mwanariadha wa Ethiopia aliyejulikana kama Koki Fai ambaye inasemekana alitoroka nchini baada ya tukio hilo.

Mwanariadha huyo ni Mkenya lakini anagombea taifa la kigeni.

Mwili wake ulipatikana katika nyumba ya mwanamume huyo huko Lillys Estate nje kidogo ya mji.

Wanariadha wenzao waliwaarifu polisi baada ya anayedaiwa kuwa muuaji kupiga simu kutoka nje ya nchi akisema alikuwa amefanya mauaji hayo.

Polisi wamefunga eneo la tukio na kwa sasa wanachunguza mazingira ya mauaji hayo.

Mkuu wa polisi wa Keiyo Kaskazini Tom Makori anaongoza timu ya maafisa ambao wako katika eneo la tukio.

Haya yanajiri miezi michache baada ya mwanariadha Agnes Tirop kuuawa katika mji huo huo Oktoba mwaka jana.