(Video) Wakenya wang'ang'ania maziwa, yoghurt baada ya lori kupata ajali

Muhtasari

• Wakenya waiba maziwa na mtindi baada ya lori la kubeba bidhaa hiyo kupinduka na kupiniria katika tambarare za Kapiti katika barabara ya Mombasa

Video moja ambayo ilipakiwa kwenye mtandao wa Twitter na mtumiaji mmoja wa mtandao huo kwa jina la Mzolex Mzolex au @Vmzolex inaonesha makumi ya watu waking’ang’ania maziwa baada ya gari lililokuwa likisafirisha maziwa hayo kupata ajali ya barabarani.

Kulingana na maelezo kwenye mkanda huo wa video, gari hilo la kampuni ya kutengeneza bidhaa mbalimbali kutokana na malighafi ya maziwa ya Brookside lilipata ajali katika eneo la Kapiti katika barabara kuu ya Nairobi-Mombasa na hapo wakaaji wa eneo hilo wakapata zawadi ya bwerere ya bidhaa hiyo ambayo imeadimika kama mkojo wa kuku ashakum si matusi.

Kitendo hicho cha kutia huruma kutoka kwa wananchi kinaashiria wazi jinsi mamia ya Wakenya wanavyoteseka na makali ya njaa ambapo wanang’ang’ania kuwahi pakiti za maziwa utadhani mbwa wanapigania kuguguna mfupa.

Inasemekana hata maafisa wa polisi waliofika katika eneo la tukio hawangeweza kuwatawanyisha wananchi hao kwani kila mmoja alikuwa na ari ya kuwahi japo kipakiti kimoja cha bidhaa hiyo adimu ambayo bei yake imekwea bei hadi ngazi za juu ambazo mwananchi wa kawaida hana uwezo tena wa kumudu kuipata.

Hakuna aliyejali kujua kama waliokuwemo ndani ya lori hilo wapo salama au la kwani kila mtu aliyekuwa na nguvu zake na uwezo alikuwa anaweka macho yake na malengo yake kwenye kuwahi maziwa.

“Nyakati ngumu na nyakati za kukata tamaa zataka hatua za kukata tamaa, Wakenya wakiiba maziwa na mtindi baada ya lori la Brookside kupinduka na kupiniria katika tambarare za Kapiti katika barabara ya Mombasa, hata hawahifadhi kreti,” mmoja mwenye alipakia video hiyo pia aliandika.

Ama kwa hakika Wakenya wamefika kiwango cha kutamauka sana mpaka kupigania bidhaa katika ajali ya barabarani badala ya kuweka jitihada za kuwaokoa waliokwama ndani mwa lile lile gari ambalo limehusika katika ajali hiyo.

Kutamaushwa huku kwa maisha kulidhihirika wazi kutokana na maaoni ya wale ambao waliachia maoni yao kwenye video hiyo ambapo idadi kubwa walikuwa wanajuta laity wangalikuwepo kwenye eneo la tukio basi wangepata bidhaa za kusitiri staftahi yao kwa muda wa siku kadhaa za kuhesabu.

Ni kubaya!