Kwa mara nyingine tena ajali mbaya imetokea katika barabara kuu ya Waiyaki jijini Nairobi, katika eneo la Brookside ambapo barabara ya Expressway inaanzia.
Ajali hiyo ambayo ilitokea Jumatano alfajiri ilihusisha gari la kubebea abiria 33 la kampuni ya Super Metro ambalo lilogonga ukuta na barabara na kupenduka kwenda barabara ya Expressway.
Ajali hiyo inaarifiwa kutokea kutokana na utepetevu wa dereva ambaye alikuwa akiendesha kwa kasi ya ajabu, jambo lililopelekea gari kupoteza mwelekeo na kupingiria mara kadhaa, hadi kufunga kiingilio cha Expressway.
Waliofika katika eneo hilo waliripoti kwamba abiria kadhaa walijeruhiwa lakini kwa bahati mbaya taniboi alisemekana kufa papo hapo.
Ajali hii inaokea katika kiingilio cha Expressway siku moja tu baada ya ajali nyingine iliyolihusisha basi la abiria 33 pia kupoteza mwelekeo na kugonga gari jingine katika kituo cha kulipa ada ya kutumia Expressway maeneo ya Mlolongo.
Eneo la Mlolongo limetajwa kuwa hatari, haswa baada ya ajali nyingine kutokea wiki mbili zilizopita katika kituo hicho cha kulipa ada cha ya matumizi ya Expressway ambayo ilihusisha gari dogo lililokuwa na mwendo wa kasi ambalo liligonga magari kadhaa na kusababisha kifo cha dereva wake.
Ajali inayohusisha magari ya uchukuzi wa umma katika barabara ya Expressway zimezua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii Jumanne, haswa baada ya baadhi ya watu kuibua wasiwasi wao kuhusu magari hayo kuruhusiwa kutumia barabara hiyo iliyoigharimu serikali kiasi kikubwa cha fedha.
Watu waligawanyika katika makundi mawili, baadhi wakihisi magari ya uchukuzi wa umma yanaendeshwa na madereva watepetevu na hivyo hayafai kuruhusiwa kutumia barabara hiyo huku wengine wakisema, barabara hiyo iko wazi kwa matumizi ya magari yote ili kuchangia ongezeko la kipato kutokana na matumizi, kipato ambacho kitasaidia serikali kufanikisha katika kulipa madeni ya mikopo iliyofadhili ujenzi wa barabara hiyo.