Mgombea urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga hatimaye amejitokeza na kuibua madai kuwa matokeo ya urais yaliyotolewa Jumatatu jioni na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ni batili.
Akizungumza katika ukumbi wa Bomas siku ya Jumanne, Raila alisema kuwa Chebukati hana mamlaka kamili dhidi ya makamishna wengine.
Alisema hatua za Chebukati kutangaza matokeo bila kuwashirikisha makamishna wote na kuwa na makubaliano ni za kidikteta. Alidai kuwa mwenyekiti huyo wa tume angeweza kusababisha vurugu nchini.
"Angeweza kuingiza nchi katika machafuko. Kutokujali huko kunaweza kuwa tishio kwa usalama. Sio juu yetu kubaini iwapo Chebukati amefanya uharamu," alisema.
Waziri huyo mkuu wa zamani aliwapongeza makamishna wanne wa tume hiyo ya kusimamia uchaguzi waliopinga matokeo huku akibainisha kuwa, kama wao makamishna hao pia waliona dosari katika mchakato wa uchaguzi.
"Wanne walipinga hatua hiyo... Makamishna walitoka nje. Takwimu zilizotangazwa na Chebukati ni batili na lazima zifutiliwe mbali na mahakama."
Raila alitangaza kuwa atachukua hatua ya kuelekea mahakamani kupinga matokeo hayo ambayo yaliashiria Ruto kuwa rais mteule.
"Hatutakubali mtu mmoja ajaribu kuleta vurugu katika taifa letu na kubadilisha yale ambayo Wakenya wameamua kama watu moja. Wakenya hawatakubali, hatutakuli. Tutazidi kutetea nchi yetu na katiba letu kama Wakenya ili Kenya iweze kuenda mbele,"
Mnamo Jumatatu, Chebukati alimtangaza Ruto mshindi baada ya kupata kura 7,176,141, dhidi ya mpinzani wake wa karibu Raila aliyepata kura 6,942,930 ambayo ni asilimia 48.85 ya kura.
Ruto alipata zaidi ya asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika kaunti 39, na kupita idadi ya chini ya kaunti 24 zinazohitajika na Katiba.
Raila alipata asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika kaunti 34.
Chebukati amemtangaza Ruto kuwa rais mteule kufuatia matokeo hayo. Makamishna wanne wa IEBC wamepinga matokeo ya uchaguzi wa urais.