Rais Ruto amfuta kazi PS wa afya Josephine,bodi ya Kemsa

Wakati uo huo Ruto amemteua Irungu Nyakera kuwa mwenyekiti wa bodi ya KEMSA.

Muhtasari
  • Ruto Jumapili aliahidi kuchukua hatua kali kufuatia madai ya kashfa kuhusu usambazaji wa neti.
Rais William Ruto
Rais William Ruto
Image: Facebook

Rais William Ruto amemfuta kazi Waziri wa Afya Josephine Mburu na bodi nzima ya shirika la KEMSA.

Ruto alikuwa siku ya Jumapili ameahidi kuchukua hatua kali kufuatia madai ya kashfa kuhusu usambazaji wa neti za kuzuia mbu.

Wakati huo huo rais alimeteua Irungu Nyakera kuwa mwenyekiti wa bodi ya KEMSA.

Waziri wa Afya Susan Nakhumicha kwa upande wake ameunda upya bodi ya Kemsa na kuteua wanachama wapya.

Wanachama hao wapya ni pamoja na Hezborn Oyieko Omollo, Bernard Kipkirui Better, Jane Masiga na Jane Nyagaturi Mbatia.

Nakhumicha wakati pia amempiga kalamu afisa mkuu mtendaji wa KEMSA Terry Ramadhani na kumteua Andrew Mutava Mulwa kama kaimu Mkurugenzi.

Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari Ikulu siku ya Jumapili, Ruto bila kufichua maelezo zaidi alisema ameanza kuangalia matatizo ya Kemsa.

"Ninafanya jambo kuhusu hilo. Utaona matokeo. Ninataka kukupa ahadi yangu, nitasafisha KEMSA, chochote kinachohitajika, chochote kinachogharimu," alisema.

Kemsa imeendelea kuteka vichwa vya habari kuhusu ufisadi na usimamizi mbovu.

Sakata ya kwanza ilikuwa takriban Sh7 bilioni zilizokusudiwa kununua vifaa vya kinga ya kibinafsi (PPE)  na muhimu vya afya katika kilele cha janga la Covid-19 na kuishia kwenye mifuko ya watu wachache waliounganishwa vizuri.