Afueni kwa Wakenya huku bei ya petroli yapunguka kwa Sh7, dizeli kwa Sh5

Bei mpya za mafuta zitaanza kutumika kuanzia usiku wa manane.

Muhtasari

•Bei ya lita moja ya dizeli kwa Sh5.09 na ya mafuta taa kwa Sh4.49 katika bei mpya ambazo zilitangazwa Alhamisi, Machi 15.

Image: BBC

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) imetangaza kupungua kwa bei ya lita moja ya petroli kwa Sh7.21.

Serikali pia imepunguza bei ya lita moja ya dizeli kwa Sh5.09 na ile ya mafuta taa kwa Sh4.49 katika bei mpya zilizotangazwa Alhamisi, Machi 15.

Katika mapitio ya kila mwezi kwa kipindi cha kuanzia saa sita usiku wa Machi 15,  gharama ya mafuta yanayotua kutoka nje iliongezeka kwa asilimia 5.6 hadi $ 703 ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Kufuatia tangazo hilo, lita moja ya petroli jijini Nairobi itauzwa kwa Sh199.15, dizeli kwa Sh190.38 huku mafuta ya taa yakiuzwa kwa Sh188.74.

Mapema siku ya Alhamisi, Rais William Ruto alikuwa amedokeza kuhusu kupungua kwa bei ya mafuta wakati akizungumza mjini Kericho. 

Katika hotuba yake, rais Ruto alisema kuwa Wakenya wangepokea habari njema kuhusu bei ya mafuta itakapotangazwa baadaye. 

Rais aliyasema hayo alipokuwa akiwahakikishia wakazi wa Kericho kwamba aliomba fursa ya kurekebisha uchumi na amefanya hivyo haswa. 

Alisema mambo mengi ya uchumi yanaonekana kuwa bora zaidi ikiwa ni pamoja na shilingi ya Kenya, ambayo sasa inaimarika dhidi ya Dola ya Marekani. 

"Mimi nilieleza mnipatie nafasi kidogo ninyoroshe hii uchumi. Kidogo ilikua imeingia kwa mtaro. Sasa nimetoa kwa mtaro hata mambo ya Dola mnaona vile inaanza kushika laini.

Na leo mtatangaziwa mambo ya mafuta imeanza kwenda laini kwa sababu tuanataka kusaidia kwamba kenya inasonga mbele bila laini ya mzingo na hatari ya mambo ya madeni. Lazima tuwe makini kama taifa," Ruto alisema.