Mahakama yaamuru Rigathi Gachagua kusalimisha Sh200M kwa Serikali

Jaji alikubaliana na malalamishi kuwa pesa hizo ni mapato ya uhalifu.

Muhtasari

•Rigathi Gachagua ameagizwa kusalimisha Sh200 milioni zilizo katika akaunti yake iliyofungiwa kwa serikali

•Mahakama  ilisema hakuna ushahidi wa kuonyesha Gachagua alikuwa na mkataba wowote na serikali kama alivyodai.

Mbunge wa Mathira Nderitu Gachagua
Mbunge wa Mathira Nderitu Gachagua

Mgombea mwenza wa UDA Rigathi Gachagua ameagizwa kusalimisha Sh200 milioni zilizo katika akaunti yake iliyofungiwa kwa serikali.

Alhamisi Jaji wa mahakama ya Milimani Esther Maina alisema alisema kwamba amekubaliana na malalamishi  kuwa pesa zinazohusika ni mapato ya uhalifu na kwa hivyo serikali inaweza kuzichukua.

Gachagua alikuwa amekiri kupokea pesa hizo kutoka kwa mashirika ya serikali baada ya kupata kandarasi.

Lakini mahakama ilisema hakuna ushahidi wowote wa  kuonyesha kuwa Gachagua  alikuwa na mkataba wowote na serikali.

Kulingana na mahakama, Gachagua aliwasilisha barua moja pekee iliyoandikwa Februari 9, 2015  kutoka kwa wizara ya serikali ikionyesha kwamba Wamunyoro Investments Ltd ilikuwa imepewa zabuni.

Lakini mbunge huyo wa Mathira hakutoa chochote cha  kuonyesha kuwa zabuni hiyo ilitekelezwa. 

Mahakama pia ilitupilia mbali madai kwamba fedha hizo zilikuwa kwenye akaunti ya amana. 

“Kulikuwa na madai kwamba fedha hizo zilikuwa kwenye akaunti ya kudumu lakini huo si ukweli,” alisema Jaji 

Fedha hizo zilizo katika Benki ya Rafiki Micro Finance, ziko katika akaunti nne. Akaunti moja ina Sh165 milioni, nyingine Sh35M na nyingine Sh773,228. Akaunti zote tatu zimesajiliwa kwa jina la Gachagua.

Akaunti ya nne, yenye Sh1,138,142, imesajiliwa kwa jina la Jenne Enterprises, mshirika wa kibiashara wa Gachagua.

Shirika la Urejeshaji Mali lilitaka pesa hizo kuwasilishwa kwa serikali kwa madai kuwa ni mapato ya uhalifu.

Shirika hilo lilikuwa limetupilia mbali madai kuwa Sh200 milioni ambazo linataka Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua na mshirika wake wa kibiashara kunyang'anywa ni kutokana na zabuni waliyoshinda miaka saba iliyopita.

Lilisema hakuna ushahidi hata kidogo wa kuunga mkono madai yaliyotolewa na Ann Kimemia aliyefanya kazi kama Jenne Enterprises Limited.

“Madai kwamba wawili hao wanafanya biashara halali na fedha zinazotolewa zinapatikana kwenye biashara halali si sahihi, ni za udanganyifu na ni mbinu ya kuficha, kuficha na kuficha chanzo cha fedha hizo. Ni mpango wa kitambo wa utakatishaji fedha," ARA inasema