logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwisho wa safari! IEBC yafutilia mbali kibali cha Sonko kuwania ugavana Mombasa

IEBC imebainisha kwa gavana huyo wa zamani wa Nairobi kuwa hawezi kukata rufaa nyingine

image
na Samuel Maina

Habari18 July 2022 - 09:30

Muhtasari


  • •IEBC ilisema uamuzi huo umefikiwa kufuatia uamuzi wa mahakama ya juu kwamba hangeweza kushikilia wadhifa wowote wa umma kutokana na kuondolewa kwake.
  • •Msimamizi wa uchaguzi katika kaunti ya Mombasa Swalhah Ibrahim amebainisha kwa gavana huyo wa zamani wa Nairobi kuwa hawezi kukata rufaa nyingine.
Gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko

Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC)  imefutilia mbali cheti cha Mike Sonko cha kuwania ugavana Mombasa.

Katika taarifa ya Jumatatu, IEBC ilisema uamuzi huo umefikiwa kufuatia uamuzi wa mahakama ya juu kwamba hangeweza kushikilia wadhifa wowote wa umma kutokana na kuondolewa kwake.

"Kwa kuzingatia hukumu ya Mahakama ya Juu zaidi kwa hivyo huna sifa ya kushikilia wadhifa wowote wa umma na hivyo basi kufutiliwa mbali kugombea na kuchaguliwa kuwa gavana wa Mombasa au kaunti yoyote ile. Uwaniaji wako umebatilishwa na cheti chako kufutiliwa mbali," Barua ya tume hiyo ilisoma.

Katika barua hiyo, msimamizi wa uchaguzi katika kaunti ya Mombasa  Swalhah Ibrahim Yusuf alibainisha kwa gavana huyo wa zamani wa Nairobi kuwa mahakama kuu ilikuwa imeamuru kusajiliwa kwake kama mgombea ugavana kufuatia kesi aliyokuwa amewasilisha katika mahakama ya juu. Aidha amemweleza kuwa hawezi kukata rufaa nyingine.

"Kwa kuzingatia ukweli kwamba mahakama ya upeo ndio mahakama ya juu zaidi kwa mujibu wa urithi wa mahakama, hakuwezi kuwa na rufaa nyingine na kwa hakika hakuna yoyote kwa sasa," Yusuf aliandika.

Ijumaa mahakama ya juu ilitupilia mbali rufaa ya Sonko kuhusu kung'atuliwa kwake mamlakani wakati akihudumu kama gavana Nairobi.

Mahakama hiyo ilishikilia maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, ikithibitisha kuondolewa kwa gavana huyo wa zamani.

Katika uamuzi huo, mahakama kuu ilikubaliana na maamuzi ya mahakama ya chini ya kuunga mkono kuondolewa kwake afisini na Seneti.

Majaji saba wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome walisema walitupilia mbali rufaa ya Sonko kwa kukosa mamlaka ya kushughulikia swala hilo.

Mahakama ya Juu ilisikiliza rufaa hiyo ambapo pande zote zilipinga kesi zao huku Sonko akisisitiza kuwa kuondolewa kwake hakukuafikia vigezo vilivyowekwa chini ya Katiba.

Rufaa hiyo ilisikizwa siku moja tu baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)kumuidhinisha kuwania kiti cha Gavana wa Mombasa katika uchaguzi wa Agosti.

Mnamo Desemba 3, 2020, Sonko alitimuliwa na Wakilishi wadi 88 wa Bunge la Kaunti ya Nairobi.

Kesi hiyo baadaye ilipelekwa kwa Seneti, kama inavyotakiwa na Katiba mnamo Desemba 17, 2020, ambapo waliidhinisha azimio la kumwondoa afisini.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved