Kura ya maoni: Nani anafaa kuwa mgombea mwenza wa William Ruto?

Muhtasari

• Wanasiasa mbalimbali wamependekezwa kuwa naibu wa William Ruto.

• Asilimia kubwa ya viongozi hao ni kutoka eneo la Mlima Kenya.

Huku siku rasmi ya uchaguzi ikizidi kukaribia kwa kasi, nafasi ya mgombea mwenza wa William Ruto inazidi kuwa kitendawili kikubwa.

Viongozi mbalimbali wamependekezwa kuchukua nafasi hiyo huku asilimia kubwa ikiwa kutoka eneo la Mlima Kenya.

Musalia Mudavadi anaongoza orodha hiyo kwa asilimia 24.2 huku mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua anafuata kwa asilimia 20.2.

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro anachukua nafasi ya tatu kwa asilimia 11.3 huku Martha Karua akifunga nne bora kwa asilimia 10.5.

Mbunge wa Gatundu kusini na kiongozi wa Chama cha Kazi, Moses Kuria ni wa tano kwa asilimia 6.5.

Huku siku rasmi ya wagombea wa kiti cha urais kutangaza wagombea wenza ikiwa Aprili 28, naibu rais William Ruto amesema kwamba atakuwa anaandaa mkutano wiki kesho ili kufanikisha mchakato wa kutafuta atakayekuwa mgombea mwenza chini ya muungano wa Kenya Kwanza.

Aidha, kumekuwa na tetesi nyingi kutoka kwa viongozi mbalimbali kwamba iwapo Ruto atashinda uchaguzi huo lazima naibu wakeatoke katika eneo la kati mwa Kenya.

Wengine pia wamedadisi kwamba Ruto anapaswa kuchagua mgombea mwenza wa jinsia ya kike.