Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi ameamuru mafisa wa trafiki kuendesha msako wa magari
yasiyostahili barabarani ili kuhakikisha usalama wa Wakenya barabarani katika
msimu wa sherehe za Krismasi.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, mkuu huyo wa mawaziri
amewataka maafisa wa usalama kuhakikisha magariyote ya uchukuzi wa umma yanamiliki
jina la ushirika wa magari, vyeti vya ukaguzi kutoka kwa mamlaka ya usafiri na
usalama barabarani NTSA pamoja na kuhakikisha kuwa magari hayo yanahudumu
katika barabara ambazo yameidhinishwa.
Mudavadi katika taarifa yake, ameelezea kusikitishwa na
ongezeko la visa vya ajali akirejelea ajali ya Jumatano ambapo watu 13
walipoteza maisha yao kwenye ajali ya barabarani katika barabara ya Kakamega –
Kisumu iliyofanyika katika eneo la Iguhu ambapo gari la kusafirisha liligonga
magari mawili ya uchukuzi wa umma.
Waziri Mudavadi amewasihi watuamiaji wote wa barabara kuwa
makini kila wanaposafiri haswa wakati huu mitihani ya kitaifa kwa shule za
sekondari inaendelea na Wakenya wanapojiandaa
kwa sherehe za Krisimasi.
Akirejelea pia takwimu za visa vya ajali katika mwaka wa
2024, waziri Musalia Mudavadi amesema kuwa inasikitisha kuwa watu 4,047
wamepoteza maisha yao kupitia ajali za barabarani kuanzia Januari hadi Novemba
wengi wa waatjiriwa wakiwa watumiaji wa barabara wa pikipiki na miguu.
Kutokana na ongezeko la visa vya ajali ikilinganishwa na mwaka jana, Musalia amewataka waendeshaji magari na pikipiki kuhakikisha wanaendesha vyombo vyao vya usafiri kwa umakini. Vile vile, ametaka magari ya usafiri wa umma yanatekeleza sheria kuambatana na sheria za usalama barabarani.
Aidha katika takwimu za ajali za mwaka 2024 kufikia Novemba, ajali 20,369 zimerekodiwa ikilinganishwa na ajali 19,262 zilizorekodiwa mwaka jana.Katika rekodi hiyo, watu 10,124 walipata majeraha makubwa katika mwaka wa 2024 ikilinganishwa na idadi ya watu 9.059 wa mwaka 2023.