Rais William Ruto amesema kuwa serikali imekuwa ikiona mahangaiko Wakenya wamekuwa wakipitia katika kipindi kigumu cha uchumi kilichoshuhudiwa ndani ya mwaka 2024.
Akizungumza mbele ya kikao cha pamoja cha bunge katika majengo ya bunge Alhamisi adhuhuri, rais Ruto amesema kuwa uchumi wa Kenya umeimarika tangu alipoingia ofisini mwaka wa 2022 baada ya uchaguzi mkuu uliopita.
Kwa mujibu wa rais Ruto, viashiria vya uchumi vinaonyesha kuimarika kwa uchumi nchini na sasa uchumi wa nchi umechukua mkondo wa kuimarika.
“Hatujakuwa tukitazama bila msaada na kutofanya chochote wakati shida ziliathiri uchumi. Viashiria vya uchumi sasa vinaelekeza mabadiliko chanya na mwelekeo wa juu zaidi.” Alisema rais Ruto.
Katika maswala ya ukuaji wa uchumi kwa mujibu wa rais Ruto, thamani ya shilingi ya Kenya imearika kwa asilimia 20 dhidi ya dola ya Marekani. Rais Ruto amesema kuwa thamani imeongezeka ambapo awali ilikuwa shilingi 162 kwa dola dhidi ya shilingi 129 dhidi ya dola sasa.
Pia, rais amesema kuwa mfumuko wa bei nchini umepungua maradufu kutoka asilimia 9.6 mnamo Septemba mwaka 2022 na kufikia Oktoba mwaka huu, mfumuko wa bei umepungua hadi asilimia 2.7. Rais Ruto amesema kuwa kupungua kwa asilimia hiyo ndio ya chini zaidi katika rekodi ya mfumuko wa bei ndani ya miaka 17 iliyopita.
Mbali na mfumuko wa bei, kwenye hotuba ya rais imebainika kuwa ubadilishaji wa fedha za kigeni uliongezeka kutoka dola bilioni 7.1 hadi dola bilioni 9.5 ikiwa ni kiwangi cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka kumi.
Vile vile, mapato ya kodi yanayokusanywa na mamlaka ya
ukusanyaji kodi nchini KRA iliimarika katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024 kwa
asilimia 11.5 kutokana na kutanuka kwa mfumo wa kusanyaji kodi. Pia rais
amesema kuwa pato la taifa liliimarika kwa uchumi wa Kenya kurekodi ongezeko la
asilimia 5.6 katika mwaka wa 2023 ikitarajiwa kuwa pato hilo litaongezeka kwa
asilimia 5 katika mwaka wa 2024 na asilimia 6 mwaka wa 2026.