Mshukiwa na unyayasaji wa kijinsia katika kaunti ya Nakuru amejiwasilisha katika mikono ya polisi kwenye kituo cha polisi cha Nakuru siku chache baada ya kudaiwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya mkewe.
Kwa mujibi wa polisi mapema Jumatatu asubuhi, mshukiwa kwa jina Elias Mutugi Njeru aliyekuwa mafichoni alijiwasilisha kwa polisi akiwa ameandamana na wakili wake Gakuhi Chege pamoja na mawakili washirika.
Kujisalimisha kwa mshukiwa huyo, kunajiri baada ya polisi kutangaza msako wa kumtafuta huku ikimtaka kujiwasilisha mwenyewe ili sheria kuchukua mkondo wake. Elias Njeru ambaye ni mtumishi katika kanisa moja jijini Nakuru, anadaiwa kumshambulia mkewe kwa kisu na kumwacha na majeraha. Kisa cha kumshambulia mkewe kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Menengai.
Mwathiriwa aliyeshambuliwa Ijumaa anaendelea kupokea matibabu katika hospitali moja jijini Nakuru kutokana na maumivu aliyoyapata aliposhambuliwa na mumewe.
Viongozi mbali mbali akiwemo gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru awali walikuwa wameshinikiza kukamatwa kwa mshukiwa huyo kutokana na uvamizi kwa mkewe wakitaka asasi za usalama kuhakikisha haki kwa mwathiriwa inapatikana. Haya yanajiri wakati ambapo serikali imetenga shilingi milioni mia moja kwa ajili uya kuendesha kampeni ya kuhamasisha wananchi dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia haswa katika mauaji ya wanawake ambayo yamekithiri.
Mshukiwa atafunguliwa mashtaka ya jaribio la kuua. Mshukiwa
huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nakuru akisubiri kufikishwa katika
kituo cha polisi cha Menengai ambapo kisa cha uvamizi kwa mkewe kiliripotiwa.