Chama cha madaktari nchini KMPDU kimedhibitisha kufariki kwa mwanafunzi wa udaktari katika hospitali ya Thika Level 5.
Kwa mujibu wa KMPDU, mwili wa mwanafunzi huyo ulipatikana asubuhi mnamo Jumatano ikidaiwa kuwa mwanafunzi huyo alipoteza maisha yake kwa kujitoa uhai.
KMPDU imesema kuwa marehemu anayetambulika kama Dkt. Francis Njuki, alikuwa mfamasia katika hospitali ya Thika level 5 na alianza kufanya kazi katika hospitali hiyo kuanzia Agosti mwaka wa 2024.
Kufariki kwa mwanafunzi huyo wa udaktari kwa njia kujitoa uhai, kinakuwa kisa cha pili ndani ya miezi miwili kwa vifo vya wanafunzi wa matibabu kutokea nchini Kenya. Mnamo mwezi Septemba, mwanafunzi mwingine wa matibabu kwa jina Desiree Moraa alipoteza uhai wake kwa njia iliyodaiwa kuwa kujitia kitanzi. Katika kisa hicho, maafisa walisema kuwa Moraa aliwacha ujumbe wa kuashiria kuwa alikuwa na msongo wa mawazo na kufanya kazi nyingi.
Katibu mkuu wa chama cha madaktari na mafamasia nchini KMPDU, Davji Bhimji Atellah, kupitia ujumbe wa barua kwa ukurasa wa KMPDU wa X, ameelezea wasiwasi wa wanafunzi madakatari kujitoa uhai akisema kuwa tayari anafahamu visa vitano vya majaribioya wanafunzi wa matibabu kutaka kujitoa uhai ila waliokolewa na kulazwa hospitalini kwa matibabu.
Chama hicho aidha kimenyooshea kidole cha lawama serikali
kikidai kuwa wanafunzi wa udaktari walioko kazini hawana mshahara. Kwa mujibu
wa katibu mkuu wa KMPDU, ameitaka serikali kuwalipa madaktari wanagenzi mishahara
yao kwa mujibu wa mkataba ulioafikiwa miaka saba iliyopita.
Uongozi wa KMPDU umesema kuwa utafanya kikao na
vyombo vya habari Jumatano kuweka wazi hatua watakazochukua.