logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Wizara ya afya yatoa pesa za kulipa wanagenzi baada ya KMPDU kutishia kuandaa mgomo

KMPDU ilitishia kutangaza notisi ya mgomo siku ya Jumamosi Novemba 30, baada ya kuwaondoa wanafunzi wa matibabu hospitalini

image
na Brandon Asiema

Hivi Punde30 November 2024 - 11:02

Muhtasari


  • Wizara ya afya imesema  kutolewa kwa fedha hizo ni hatua muhimu katika kujitolea kwa serikali kuwasaidia wataalamu wa afya wanapoanza kujijenga kitaaluma pamoja na kuimarisha mfumo wa afya nchini.
  • KMPDU awali ilikuwa imeonya kwamba ikiwa serikali ingalikosa kuchukua hatua kushughulikia swala hilo, ingalilaumiwa kwa maafa ambayo yangalitokea ikiwa huduma za matibabu zingalisitishwa nchini kote.


Siku chache baada ya muungano wa madaktari nchini KMPDU kuwaondoa madaktari wanagenzi kazini hadi wakati serikali itajukumika kulipa mishahara kwa wanagenzi hao, hatimaye serikali kupitia wizara ya afya imetangaza kutoa shilingi 965,875,345.60 kwa malipo ya wanagenzi hao.

Kwa mujibu wa wizara ya afya, hela hizo zimetolewa ili kugharamia malipo ya kila mwezi yaliyokuwa yanadaiwa na wanagenzi katika idara ya nesi, maafisa wa kliniki, maafisa wa matibabu  na wanafamasia.

Wizara hiyo imesema kwamba kutolewa kwa fedha hizo ni hatua muhimu katika kujitolea kwa serikali kuwasaidia wataalamu wa afya wanapoanza kujijenga kitaaluma pamoja na kuimarisha mfumo wa afya nchini.

Mnamo Jumatano, Novemba 27, KMPDU kwenye mtandao wake wa X, iliwataka wanagenzi wa utibabu kutoripoti kazini hadi serikali itakapowajibika ikitishia kutoa ilani ya mgomo Jumamosi ikielezea madhila wanayopitia.

Hata hivyo, huenda ilani ya mgomo ilipangiwa kutolewa Jumamosi Novemba 30, ikatupiliwa mbali baada ya wizara ya afya kutoa hela za malipo kwa wanagenzi hao.

KMPDU awali ilikuwa imeonya kwamba ikiwa serikali ingalikosa kuchukua hatua kushughulikia swala hilo, ingalilaumiwa kwa maafa ambayo yangalitokea ikiwa huduma za matibabu zingalisitishwa nchini kote.

Wizara ya afya imetangaza kwamba shilingio 528,615,125.60 zimetolewa kwa ajili ya kulipa madeni zilizokuwa zinadaiwa huku shilingi 110,668,070 zikitolewa kwa madaktari wanagenzi ambao ni manesi na maafisa wa kliniki. Vile vile, shilingi 326,592,150 zimetolewaili kulipa madeni kwa wanagenzi madaktari kwenye idara za maafisa wa matibabu, daktari wa meno na wanafamasia.

Kuondolewa kwa madaktari wanagenzi na muungano wa madaktari kulijiri baada ya kisa cha pili ya mwanagenzi wa udaktari kufariki kwa kujitoa uhai KMPDU ikinyooshea kidole cha lawama serikali kuwa chanzo cha kisa kutokana na kutowalipa wanagenzi kwa muda mwafaka. Kisa hicho cha mwanafamasia katika hospitali ya Thika Level 5 kilijiri miezi miwili baada ya mwanagenzi mwingine kwenye taaluma ya matibabu kujitoa uhai kwa kujinyionga katika eneo la Gatundu kwa madai hayo hayo.

Hata hivyo, wizara ya afya imeelezea kujitolea kwake katika kusulihisha masuala katika sekta ya afya ikiahidi kuwa changamoto za aina hiyo hazijirudii tena katika siku za usoni.

“Wizara ya afya bado imejitolea kutatua masuala yoyote ambayo hayajashughulikiwa na kuhakikisha kuwa changamoto kama hizo hazitokei katika siku zijazo.” Wizara ya afya ilisema katika ujumbe wake kwa vyombo vya habari.

Kutokana na kutolewa kwa fedha hizo, wizara ya afya imewataka wanagenzi wote kurejea katika idara zao husika.



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved