Wafanyakazi wa mashamba ya mpunga 'wachinjwa' Nigeria

Wakulima 43 wamezikwa Jumapili. (Picha: BORNO STATE GOVERNMENT)
Wakulima 43 wamezikwa Jumapili. (Picha: BORNO STATE GOVERNMENT)

Wananchi wapatao 110 wameuawa nchini Nigeria na wengine kujeruhiwa katika shambulio la wakulima kaskazini mwa Nigeria. Mratibu wa Umoja wa Mataifa -UN Edward Kallon,ametoa taarifa hiyo siku ya Jumapili.

Awali ripoti zilisema wakulima wapatao 40 waliuawa wakati wa shambulio hilo katika mashamba ya mpunga karibu na mji wa Maiduguri.

Taarifa mpya zinaonesha kuwa idadi ya waliouawa ni kubwa zaidi ya ile iliyotajwa na mamlaka ya Nigeria.

Kwa mujibu wa mratibu wa UN nchini Nigeria, Edward Kallon, amesema wanaume waliokuwa katika pikipiki waliwashambulia wakulima hao waliokuwa wanavuna mpunga huko Koshobe, katika jimbo la Borno.

Amelaani vikali shambulio hilo na kutaka mamlaka kutenda haki dhidi tukio hilo.

Mapema Jumapili , gavana wa Borno alitaka vijana wengi wajitokeze kusaidia kupambana na wavamizi hao katika ukanda huo.

Alisema watu karibu 43 wameuawa katika kile ambacho rais wa Nigeria anakieleza kama shambulizi la "kiwenda wazimu" lililotekelezwa kaskazini mashariki mwa Nigeria Jumamosi.

Washambuliaji waliwafunga kamba wafanyakazi wa mashamba ya mpunga na kukata koo zao karibu na eneo la Maiduguri, mji mkuu wa Borno, ripoti zinasema.

Hili lilikuwa moja ya mashambulizi mabaya zaidi katika miezi ya hivi karibuni ambako makundi ya wanamgambo wa Boko Haram na Islamic State Magharibi mwa Afrika yanatekeleza shughuli zake.

Hadi kufikia sasa hakuna aliyedia kuhusika na shambulizi hilo.

"Nalaani mauaji ya wakulima wetu ambao ni wachapa kazi yaliyotekelezwa na wanamgambo katika jimbo la Borno. Nchi nzima imeumizwa na mauaji haya. Maombi yangu ni kwa familia katika kipindi hiki kigumu cha maombelezi. Mungu alaze roho zao mahali pema peponi," amesema Rais Muhammadu Buhari.

Rais Buhari pia alielezea "mauaji hayo ya kigaidi kama uendawazimu", kulingana na msemaji wake Garba Shehu.

"Tumepata miili 43 ya watu waliokufa, wote wamechinjwa pamoja na wengine sita waliopata majeraha mabaya," afisa wa polisi wa eneo aliyesaidia walionusurika amezungumza na shirika la habari la AFP.

Baadhi ya wafanyakazi wa mashamba hayo bado hawajulikani walipo, huku mkaazi mmoja na Shirika la Amnesty International wakisema wanawake 10 ni miongoni mwao.

Waathirika wa shambulizi hilo ni wafanyakazi wa mashamba kutoka jimbo la Sokoto kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Waliofariki dunia wamezikwa Jumapili, gavana wa jimbo akihudhuria mazishi hayo. (Picha: BORNO STATE GOVERNMENT)
Waliofariki dunia wamezikwa Jumapili, gavana wa jimbo akihudhuria mazishi hayo. (Picha: BORNO STATE GOVERNMENT)

Gavana wa jimbo la Borno, Babagana Zulum, alihudhuria' mazishi ya waaathirika Jumapili.

"Inaumiza moyo kuona zaidi ya raia 40 wamechinjwa wakiwa wanafanyakazi katika mashamba yao," aliwaambia wanahabari.

"Watu wetu wanapitia kipindi kigumu sana, njia mbili tofauti: upande mmoja wakisalia nyumbani, huenda wakafariki dunia kwasababu ya njaa; na upande mwingine, wanakwenda kufanyakazi yao ya shambani na wanakuwa katika hatari ya kuuliwa na wanamgambo. Hii inasikitisha sana."

Alitoa wito kwa serikali kusajili wanajeshi zaidi na maafisa wengine wa usalama kulinda wakulima katika eneo hilo.

Wakulima hao "walishambuliwa kwasababu siku ya Ijumaa walichukua silaha za mwanamgambo mmoja wa kundi la Boko harama na kumkamata kwasababu amekuwa akiwatesa " mbunge mmoja wa eneo, Ahmed Satomi, amezungumza na gazeti la Premium Times.

Aidha, wadadisi wa mambo wanasema, wakulima hao awali, walishambuliwa na wanamgambo wa kundi la Kiislamu Boko Haram, waliowashuku kuwa wanapeleka taarifa kwa wanajeshi.

Mwezi uliopita, wapiganaji wa Boko Haram waliwaua wakulima 22 waliokuwa wanafanyakazi kwenye mashamba ya umwagiliaji maji katika matukio mawili tofauti.

Jumapili, wanajeshi sita walisemekana kuuawa na wapiganaji wa jihadi karibu na mji wa Baga jimbo la Borno, amesema mwandishi wa BBC Chris Ewokor, mjini Abuja.

Wanajeshi hao walikuwa njiani kuelekea eneo hilo kuimarisha usalama katika eneo la ugawaji wa chakula kwa watu waliohama makazi yao kwasababu ya vita.

Licha ya juhudi za eneo za kumaliza ghasia zinazotekelezwa na kundi la Boko Haram, kundi hilo limekuwa likiimarisha mashambulizi yake miezi ya hivi karibuni.

Serikali ya Nigeria imedai mara kadhaa kuwa imeyashinda nguvu makundi ya wanamgambo wa Kiislamu, wachambuzi wanasema.

Lakini jeshi la Nigeria limeonekana kushindwa kumaliza makundi hayo mbapo makumi ya maelfu ya raia wameuawa au kutekwa nyara.

BBC