Joto la siasa! Kalonzo asema Ruto ni mkabila

Muhtasari

  • Kalonzo alisema Ruto aliteua watu kutoka jamii yake pekee katika baraza la mawaziri.

  • Alidai naibu rais alichangia kuondelewa kwa waziri wa Afya Cleopa Mailu.

  • Alisema kuondolewa kwa Mailu kumeacha jamii nzima ya wakamba bila waziri katika baraza la mawaziri la sasa.

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka
Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka
Image: MERCY MUMO

TAARIFA YA LUKE AWICH 

Aliyekuwa makamu wa  rais Kalonzo Musyoka amemrushia makombora naibu rais William Ruto akimshtumu kwa kuteua watu kutoka jamii yake pekee kwa baraza la mawaziri.

Kalonzo, katika kile kinaonekana kama mashambulizi makali dhidi ya Naibu rais, alisema Ruto anapaswa kuacha kujionyesha kama mzalendo. Kinara huyo wa Wiper alisema rangi halisi ya Ruto ilifichuliwa jinsi alivyozigawa nafasi zake za asilimia 50 katika baraza la mawaziri.

Vinara watatu wa NASA Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Musalia Mudavadi katika siku chache zilizopita wamemshambulia sana naibu rais katika kile kinaonekana kama kuanza kwa joto la siasa za 2022.

 
 

Kwa mara ya kwanza, Kalonzo asiyefahamika kwa siasa za malumbano alidai kuwa Ruto alikwenda mbali hata kuwafurusha mawaziri kutoka jamii zingine ili kuwatafutia nafasi watu wake.

Kiongozi huyo wa Wiper alitoa mfano wa waziri wa zamani wa Afya Cleopa Mailu, ambaye alifungiwa nje ya Baraza la Mawaziri baada ya kuchaguliwa tena kwa serikali ya Jubilee mwaka 2017.

Balozi Cleopa Mailu amabye alikuwa waziri wa Afya
Balozi Cleopa Mailu amabye alikuwa waziri wa Afya
Image: Maktaba

“Hata Balozi Mailu angekuwa waziri leo. Nilifuatilia habari hiyo kwa karibu sana na Rais Uhuru Kenyatta na niliambiwa yeye [Uhuru] hakuwa na shida na Mailu. Angeendelea kuwa waziri, "Kalonzo alisema.

Alisema kuondolewa kwa Mailu kumeacha jamii nzima ya wakamba bila waziri katika baraza la mawaziri la sasa.

"Una jamii isiyo na waziri hata mmoja na unafikiria kweli unaweza kuja kuwachanganya Wakamba na hizo pesa za uchumi wa mikokoteni?" Makamu wa Rais wa zamani aliuliza.

“Tangu mwaka 1963 wakati nchi hii ilikuwa na Uhuru, tulikuwa na mawaziri wasiopungua wawili katika baraza la mawaziri kutoka jamii hiyo. Huu sio ukabila; ni ukweli wa hali halisi.”

Mailu kwa sasa ni balozi wa Kenya katika umoja wa mataifa huko Geneva na Mwakilishi wa Kudumu katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Geneva.

Kalonzo alisema hayo ni baadhi ya maswali magumu ambayo Ruto atakabiliwa nayo wakati atazuru kaunti ya Machakos ili kumpigia debe mgombea wake wa useneta.

Kiongozi huyo wa Wiper, ambaye pia ni mjumbe maalum wa amani Sudan Kusini, alikuwa akijibu makombora ya hivi majuzi ya Ruto kuhusu pendekezo la Rais Kenyatta kuwa jamii nyingine itoe kiongozi wa taifa.

Ruto alikuwa amesema Wakenya waruhusiwe kumchagua Rais wao kwa sifa na sera zake na sio kuzingatia kabila.

Mwishoni mwa wiki, Ruto kwa mara ya kwanza alionekana kujibizana na Rais Kenyatta, na kutaja pendekezo la rais kama la kikabila na ambalo limepitwa na wakati.