Uganda yarekodi viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya virusi vya corona

Muhtasari
  • Uganda yarekodi viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya virusi vya corona
  • Nchini hiyo imekuwa ikikabiliwa na aina mpya ya virusi ambayo viligunduliwa kwanza nchini India, Uingereza, na Afrika Kusini

Uganda imeandikisha viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya virusi vya corona kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu janga la hilo lilipoanza.

Watu 1,438 kati ya 8,478 waliambukizwa virusi kulingana na takwimu iliyotolewa na Wizara ya Afya siku ya Alhamisi. Vipimo vilifanywa tarehe 8 mwezi Juni.

Nchini hiyo imekuwa ikikabiliwa na aina mpya ya virusi ambayo viligunduliwa kwanza nchini India, Uingereza, na Afrika Kusini ikiwemo kirusi kingine kilichogunduliwa China.

Kuna wasi wasi visa vya maambukizi vinaendelea kuongezeka na hospitali huenda zikalemewa kwa kukosa vifaa tiba muhimu kama vile oksijeni.

Shirika la ndege la kitaifa la Rwanda RwandAir limesitisha safari zake kwenda Uganda kutokana na ongezeko la maambukizi.

Siku ya Jumatano, Milki ya Falme za Kiarabu zilisema kwamba wasafiri kutoka Uganda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hawataruhusiwa kuingia nchini humo kuanzia Ijumaa hii.

Zaidi ya watu 750,000 wamepewa chanjo ya corona nchini Uganda kufikia sasa.

Nchi ilikuwa imepokea dozi 964,000 za chanjo ya AstraZeneca mnamo mwezi Machi, ambayo inaelekea kuisha.