Papa Francis 'anaendelea vizuri' baada ya kufanyiwa upasuaji wa koloni

Muhtasari
  • Papa Francis amefanyiwa upasuaji wa tatizo la utumbo mkubwa au koloni uliofanikiwa katika hospitali moja huko Roma
pop
pop

Papa Francis amefanyiwa upasuaji wa tatizo la utumbo mkubwa au koloni uliofanikiwa katika hospitali moja huko Roma, Vatican imesema.

Hali ya afya ya Papa Francis, 84, "inaendelea vizuri" baada ya kufanyiwa upasuaji ambao ilibidi apigwe ‘nusu kaputi’, msemaji wa Vatican Matteo Bruni amesema.

Ni mara ya kwanza Papa Francis kulazwa hospitalini tangu kuchaguliwa kwake kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki ulimwenguni mwaka 2013.

Mapema Jumapili, Papa ambaye ni raia wa Argentina alihutubia maelfu ya wageni katika uwanja wa St Peter's.

Katika taarifa iliyotolewa awali, Vatican ilisema Papa Francis alikuwa anatibiwa katika hospitali ya chuo kikuu cha Gemelli kwa tatizo la koloni.

Ugonjwa huo ni hali inayojumuisha vifuko katika ukuta wa utumbo mpana ambako kunaweza kusababisha kupungua kwa koloni.

Dalili zake ni pamoja na tumbo kuvimba, kuwa na maumivu na mabadiliko ya tabia za utumbo.

Vatican haikutoa maelezo zaidi kuhusu upasuaji huo au kipindi ambacho Papa anatarajiwa kuwa hospitalini.

Wakati wa ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Papa alitangaza kuwa ataenda Slovakia mnamo mwezi Septemba baada ya kufanya ibada ya kusherehekea huko Budapest, mji mkuu wa Hungary.

Papa Francis mwaka 1936 huko Buenos Aires, na alipoteza sehemu ya pafu lake la upande wa kulia akiwa na umri wa miaka 21.

Pia aliwahi kupata tatizo la nyonga na siatika (ugonjwa wa mshipa wa nyuma ya paja), ambako kunasababisha uchungu kuanzia sehemu ya chini ya mgongo hadi miguuni.

Mwaka 2014, alilazimika kuahirisha shughuli zake kadhaa kwa sababu ya tatizo maradhi ya tumbo.