MAUAJI YA RAIS WA HAITI

Mshukiwa muhimu wa mauaji ya rais wa Haiti Jovenel Moïse anaswa

Polisi nchini Haiti wanasema wamemkamata daktari ambaye wanaamini ni mshukiwa mkubwa katika kupanga mauaji ya Rais Jovenel Moïse.

Muhtasari

•Bw Moïse, 53, aliuawa nyumbani kwake mnamo Julai 7 na mamluki 28 wa kigeni, polisi walisema walithibitisha hapo awali.

•Kukamatwa kwa Bw Sanon kulitangazwa katika mkutano wa polisi na wanahabari siku ya Jumapili katika mji mkuu Port-au-Prince.

Image: EPA

Polisi nchini Haiti wanasema wamemkamata daktari ambaye wanaamini ni mshukiwa mkubwa katika kupanga mauaji ya wiki iliyopita ya Rais Jovenel Moïse.

Wanasema Christian Emmanuel Sanon, raia wa Haiti mwenye umri wa miaka 63, aliingia nchini humo kwa ndege binafsi mapema Juni huku akiwa na "nia za kisiasa".

Bw Moïse, 53, aliuawa nyumbani kwake mnamo Julai 7 na mamluki 28 wa kigeni, polisi walisema walithibitisha hapo awali.

Mkewe alijeruhiwa katika shambulio hilo na kisha kusafirishwa kwenda Marekani kwa matibabu.

Martine Moïse baadaye alielezea namna wauaji "walipommiminia risasi" mumewe katikati ya usiku.

Alisema shambulio hilo lilitokea haraka sana, mumewe Jovenel hakuweza "kusema neno hata moja."

Kukamatwa kwa Bw Sanon kulitangazwa katika mkutano wa polisi na wanahabari siku ya Jumapili katika mji mkuu Port-au-Prince.

"Huyu ni mtu ambaye aliingia Haiti kwa ndege ya binafsi akiwa na malengo ya kisiasa," mkuu wa polisi wa Haiti Leon Charles alisema.

Alisema mpango wa awali ulikuwa wa kumkamata Rais Moïse, lakini "misheni hiyo ilibadilika". Hakufafanua zaidi ya hapo.

"Wakati sisi, polisi, tulizuia vitendo vya majambazi hawa baada ya kufanya uhalifu wao, mtu wa kwanza ambaye mmoja wa washambuliaji alimpigia simu alikuwa Christian Emmanuel Sanon," amesema Bw Charles.

"Aliwasiliana na watu wengine wawili ambao tunachukulia kuwa ndio wapangaji wakuu wa mauaji ya Rais Jovenel Moïse." Mkuu wa polisi hakusema hao watu wengine wawili walikuwa akina nani.

Marekani yaingilia kutathmini hali ya usalama

Ujumbe wa maafisa wakuu wa usalama wa Marekani uliwasili Haiti jana Jumapili kutathmini hali ya usalama.

Timu hiyo pia itakutana na wanasiasa watatu wa Haiti. kila mmoja kati yao anadai kuwa kiongozi halali wa nchi.

Baada ya shambulio hilo, mamlaka ya Haiti iliziomba Marekani na UN kutuma vikosi nchini humo kulinda miundombinu muhimu.

Utawala wa Rais Joe Biden hapo awali ulikataa ombi hilo - lakini sasa umeamua kuangalia kwa karibu hali hiyo.

Bwana Moïse alikuwa rais wa Haiti, taifa maskini zaidi katika Amerika, tangu 2017. Wakati wake katika ofisi mgumu na alikabiliwa na tuhuma za ufisadi na kulikuwa na maandamano mengi katika mji mkuu na miji mingine mapema mwaka huu dhidi ya utawala wake.

Uchaguzi wa bunge ulipaswa kufanywa mnamo Oktoba 2019 lakini mizozo imechelewesha kura , ikimaanisha Bw Moïse alikuwa akitawala kwa amri. Alikuwa amepanga kufanya kura ya maoni juu ya mabadiliko ya katiba yaliyopendekezwa mnamo Septemba hii.

Mjane wa rais azungumza

Mjane aliyejeruhiwa wa rais wa Haiti alielezea wakati wauaji "walipommiminia risasi" mumewe baada ya kupenya na kuingia nyumbani kwao katikati ya usiku.

Martine Moïse alisema shambulio hilo lilitokea haraka sana, mumewe Jovenel hakuweza "kusema hata neno moja."

Jumamosi, alitoa ujumbe wa sauti kwenye ukurasa wake wa Twitter akiapa kuendelea na kazi yake. Watu kadhaa wamethibitisha kuwa ujumbe huo ni wa mke wa rais.

Image: MARTINE MOISE//TWITTER

Ghafla, mamluki waliingia nyumbani kwangu na kumuua mume wangu kwa risasi," Bi Moïse anasema katika rekodi hiyo, akielezea wakati ambapo washambuliaji walimuua mumewe.

"Kitendo hiki hakina jina kwa sababu lazima uwe mhalifu sugu kumuua rais kama Jovenel Moïse, bila hata kumpa nafasi ya kusema neno moja," aliongeza

Alidai kamba mumewe alikuwa akilengwa kwa sababu za kisiasa - haswa, akitaja kura ya maoni juu ya mabadiliko ya katiba ambayo ingeweza kumpa rais nguvu zaidi.

Watu hao ambao hawajulikani alisema, "wanataka kuua ndoto ya rais".

"Ninalia, ni kweli, lakini hatuwezi kuiacha nchi ipotee," aliongeza. "Hatuwezi kuruhusu damu ya Rais Jovenel Moïse, mume wangu, rais wetu ambaye tunampenda sana na ambaye alitupenda sisi, kupita bure."

Bw Moïse, mwenye umri wa miaka 53, alikuwa rais wa Haiti, taifa maskini zaidi katika Amerika, tangu 2017. Wakati wake katika ofisi ulikuwa mgumu kwani alikabiliwa na tuhuma za ufisadi na kulikuwa na maandamano mengi katika mji mkuu na miji mingine mapema mwaka huu.

Uchaguzi wa bunge ulipaswa kufanywa mnamo Oktoba 2019 lakini mizozo imechelewesha, ikimaanisha Bw Moïse alikuwa akitawala kwa amri. Alikuwa amepanga kufanya kura ya maoni juu ya mabadiliko ya katiba yaliyopendekezwa mnamo Septemba hii.

Mnamo Februari mwaka huu, siku ambayo wapinzani walitaka aondoke afisini, Bw Moïse alisema jaribio la kumuua na kupindua serikali lilishindwa.

Bado haijulikani ni nani aliyepanga shambulio la Jumatano na kwa nia gani. Maswali kadhaa bado hayajajibiwa, pamoja na jinsi wauaji wanaodaiwa kutekeleza mauaji yake walivyoweza kuingia katika boma lake. Walinzi wa Bw Moïse wanastahili kuhojiwa wiki ijayo.

Kiongozi mmoja maarufu wa upinzani ameelezea waziwazi wasiwasi juu ya tukio hilo. Seneta wa zamani wa Haiti Steven Benoit aliambia kituo cha redio Magik9 siku ya Ijumaa kuwa "sio Wakolombia waliomuua", lakini hakutoa ushahidi kuunga mkono madai yake.

Polisi wa Haiti wamesema wengi wa mamluki walikuwa Wakolombia , wakati wawili walikuwa raia wa pamoja wa Marekani.

Kumi na saba wa kikundi hicho walizuiliwa katika mji mkuu Port-au-Prince baada ya makabiliano ya risasi. Washukiwa watatu waliuawa na polisi, na wengine wanane bado wanatafutwa.

Serikali ya Colombia imeahidi kuisaidia Haiti na juhudi zake za uchunguzi.

Mkurugenzi wa polisi wa Colombia, Jenerali Jorge Luis Vargas, alisema wanajeshi 17 wa zamani wa Colombia walidhaniwa kuhusika.

Ni nani anayeiongoza Haiti?

Katiba inasema Bunge linapaswa kuchagua rais mwingine. Lakini mizozo ilimaanisha kuwa uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 2019 haukufanyika - na Bw Moïse alikuwa akitawala kwa amri wakati maandamano yalipoenea.

Marekebisho ya katiba - ambayo hayakubaliwi na kila mtu - yanaonyesha kuwa waziri mkuu ndiye anayepaswa kuchukua nafasi hiyo.

Image: GETTY IMAGES

Lakini Haiti ina waziri mkuu wa muda, Claude Joseph, na mteule mpya, Ariel Henry, ambaye bado hajaapishwa.

Wote wanadai kuwa wapo kwenye usukani .

Siku ya Ijumaa, kikundi cha vyama vya siasa kilitia saini azimio la kumtangaza rais mpya - Joseph Lambert - na Bw Henry akishikilia nafasi ya Waziri Mkuu wake.

Hatua hiyo haijafanya mengi kutatua machafuko ya kisiasa na kiuchumi ambayo kwa muda mrefu yamelizonga taifa hilo.