Waziri wa Ulinzi nchini Tanzania afariki dunia

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini humo, Jenerali Venance Mabeyo

Muhtasari

•Waziri Kwandikwa, alikuwa akipata matibabu katika hospitali ya taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa karibu siku kumi na nne.

•Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko kifo cha waziri huyo kutokana na mchango wake mkubwa katika utumishi wa Umma.

Image: Ikulu Mawasiliano

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa nchini Tanzania, Elias Kwandikwa, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam.

Waziri Kwandikwa, alikuwa akipata matibabu katika hospitali ya taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa karibu siku kumi na nne.

Kwandikwa pia ni mbunge wa Ushetu katika mkoa wa Shinyanga.

Katibu wa Mbunge huyo, Julius Lugobi amethibitishia Mwananchi Digital kuwa Mbunge huyo ameaga dunia hapo jana.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini humo, Jenerali Venance Mabeyo, Taarifa kutoka Ikulu imeeleza.

Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko kifo cha waziri huyo kutokana na mchango wake mkubwa katika utumishi wa Umma.

‘’Tumepoteza mtu muhimu ambaye mchango wake katika utumishi wa Umma hautasahaulika, Kwandikwa alikuwa kiongozi shupavu ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu’’. Alisema Rais Samia.