Daktari asimamishwa kazi kwa kumfumua mgonjwa nyuzi baada ya kushindwa kulipia matibabu

Muhtasari

•Katika video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii imemuonesha daktari mmoja akilalamikiwa na kiongozi wa Kijiji kwa kumfumua nyuzi mgonjwa mara baada ya kumshona, kisa mgonjwa huyo alishindwa kulipa gharama za matibabu hayo.

Image: BBC

Daktari mmoja nchini Tanzania amesimamishwa kazi kwa kumfumua nyuzi mgonjwa kisa alishindwa kulipia matibabu.

Katika video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii imemuonesha daktari mmoja akilalamikiwa na kiongozi wa Kijiji kwa kumfumua nyuzi mgonjwa mara baada ya kumshona, kisa mgonjwa huyo alishindwa kulipa gharama za matibabu hayo.

Baadaye daktari huyo alitambuliwa kama Jackson Meli kutoka katika kituo cha afya Kerenge, Mkoani Tanga.

Awali mamlaka nchini Tanzania iliomba taarifa za kuweza kumtambua daktari huyo kupitia mitandao ya kijamii. Mgonjwa ambaye anaoenakana kwenye video hiyo alikuwa ameshonwa katika upande wa juu wa mkono na baadaye kufumuliwa.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Basila Mwanukuzi alikemea kitendo hicho na kusema kuwa tayari hatua za kinidhamu zimechukuliwa na taarifa zake zimefikishwa kwenye baraza la matabibu. ‘’Jambo hili lilitokea toka tarehe 28 mwezi wa saba na alikamatwa mara moja na kuwekwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi, na alisimamishwa kazi na halmashauri na taarifa zake zimewasilishwa kwenye baraza la matabibu la Tanzania’’ anasema Mwanukuzi.

Chama cha madkatari Tanzania kimekemea pia tukio hilo, katika taarifa iliyotolewa leo na kusisitiza hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake.