Mapadre wa kikatoliki Ufaransa waliwanyanyasa watoto 216,000 tangu mwaka 1950

Muhtasari

•Mapema mwaka huu Papa Francis alibadili sheria ya Kanisa Katoliki ili kuweka wazi unyanyasaji wa kingono kuwa uhalifu, yakiwa ni mabadiliko makubwa katika sheria ya uhalifu kufanyika kwa miongo kadhaa.

Image: GETTY IMAGES

Takriban watoto 216,000 wamekuwa waathiriwa wa unyanyasaji uliofanywa na mapadre wa kikatoliki nchini Ufaransa tangu mwaka 1950, mkuu wa uchunguzi wa unyanyasaji wa wajumbe wa kanisa anasema.

Jean-Marc Sauvé alikuwa akizungumza wakati alipokuwa akitoa ripoti ya kina kuhusu unyanyasaji wa kingoni katika Kanisa Katoliki nchini Ufaransa.

Amesema kwamba idadi ya waathiriwa inaweza kufikia watu 330,000, iwapo Wakristo wa kanisa hilo wangejumuishwa.

Muathiriwa ammoja ameitaja ripoti hiyo kama hatua ya mabadiliko katika historia ya Ufaransa.

Akizungungumza katika ufichuzi wa ripoti hiyo, Bw Jean-Marc Sauvé amelaani uongozi wa kanisa na akasema taasisi hiyo haifanya kazi.

Bw Sauvé, ambaye ni mfanyakazi wa umma wa ngazi ya juu nchini Ufaransa, ameliambia gazeti la Ufaransa Le Monde kwamba jopo analoliongoza lilikuwa limewasilisha ushahidi kwa waendesha mashitaka katika kesi 22 ambazo mashitaka ya uhalifu bado yanaweza kuanzishwa.

Aliongeza kuwa maaskofu na maafisa wengine wa ngazi ya juu walikuwa wamefahamishwa kuhusu madai mengine dhidi ya watu ambao bado wanaishi.

Wajumbe wa kamati hiyo ya uchunguzi walikuwa ni pamoja na wanahistoria, madaktari na wanatheolojia.

Zaidi ya waathiriwa 6,500 na mashahidi waliwasiliana na tume hiyo katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita. Ripoti ya mwisho ya uchunguzi huo ina jumla ya kurasa 2,500.

Image: EPAVATICAN MEDIA HANDOUT

Mapema mwaka huu Papa Francis alibadili sheria ya Kanisa Katoliki ili kuweka wazi unyanyasaji wa kingono kuwa uhalifu, yakiwa ni mabadiliko makubwa katika sheria ya uhalifu kufanyika kwa miongo kadhaa.

Sheria mpya inaufanya unyanyasaji wa kingono, kuwalaghai watoto wadogo, kumiliki ponografia ya watoto na kuficha unyanyasaji huu kuwa kosa chini ya sheria ya Kikatoliki.