Ufaransa inachunguza ubakaji wa askari katika ikulu ya Élysée

Muhtasari
  • Rais Emmanuel Macron alikuwa amehudhuria hafla hiyo, iliyofanyika kwa wafanyikazi wanaoondoka
  • Mtuhumiwa - pia mwanajeshi - amehojiwa, lakini bado hajafunguliwa mashtaka rasmi, ripoti zinasema
Image: BBC

Waendesha mashtaka wa Ufaransa wamefungua uchunguzi kuhusu madai ya ubakaji katika ikulu ya rais mjini Paris.

Vyombo vya habari nchini humo vinaripoti kwamba mwanajeshi wa kike amesema alinajisiwa baada ya tafrija ya vinywaji katika jumba la Élysée mwezi Julai.

Rais Emmanuel Macron alikuwa amehudhuria hafla hiyo, iliyofanyika kwa wafanyikazi wanaoondoka.

Mtuhumiwa - pia mwanajeshi - amehojiwa, lakini bado hajafunguliwa mashtaka rasmi, ripoti zinasema.

Gazeti la Libération liliripoti kwanza mashtaka hayo siku ya Ijumaa.

Wote wawili wanaodaiwa kuwa mwathiriwa na mshambulizi waliripotiwa kufanya kazi katika ofisi ya wafanyakazi wa ulinzi mkali katika jengo hilo, na Libération ilisema wanafahamiana.

Afisa wa rais aliliambia shirika la habari la AFP kwamba "mara tu mamlaka zilipofahamu madai haya, hatua zilichukuliwa mara moja" kumsaidia mwathiriwa huyo.

Yeye na mtuhumiwa wote wamehamishwa kwa majukumu mengine, ikulu ilisema.