Wafungwa 38 wafariki, 69 wajeruhiwa katika mkasa wa moto gerezani Burundi

Haijabainika ni nini kilisababisha moto huo

Muhtasari

•Kumi na wawili kati ya waliofariki walisakamwa na moshi huku 26 waliosalia wakipata majeraha ya moto,

Moto mkubwa
Moto mkubwa
Image: WIKIPEDIA

Takriban wafungwa 38 wamefariki dunia na wengine 69 kujeruhiwa katika moto ulioteketeza gereza kuu la mji mkuu wa kisiasi wa Burundi Gitega mapema Jumanne.

Haijabainika ni nini kilisababisha moto huo.

Kumi na wawili kati ya waliofariki walisakamwa na moshi huku 26 waliosalia wakipata majeraha ya moto, kulingana na makamu wa rais wa Burundi, Prosper Bazombanza, ambaye alitembelea kituo hicho na hospitali ambapo wengi wa majeruhi wanatibiwa.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa majeruhi 34 waliopata majeraha ya moto ya wastani na zaidi wamepelekwa hospitali huku wengine wakipatiwa matibabu katika eneo la gereza.

"Wafanyikazi wa afya wametupa hakikisho kwamba watapona", alisema.

Afisa huyo pia alitangaza bili yao ya matibabu italipwa kikamilifu na serikali.

Hali mbaya ya usalama ilifanya iwe rahisi kwa moto huo kuenea haraka katika gereza ambalo awali lilikusudiwa watu 400 lakini sasa lilikuwa na wafungwa zaidi ya 1500.

Kiwango kamili cha uharibifu kilikuwa bado hakijajulikana.