Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok ajiuzulu baada ya maandamano makubwa

Muhtasari

‚ÄĘKujiuzulu kwake kunafuatia siku nyingine ya maandamano, ambapo madaktari walisema takribani watu wawili waliuawa.

Abdalla Hamdok alirejeshwa tena madarakani mwezi Novemba baada ya kutia saini makubaliano ya kugawana madaraka na kiongozi wa mapinduzi
Abdalla Hamdok alirejeshwa tena madarakani mwezi Novemba baada ya kutia saini makubaliano ya kugawana madaraka na kiongozi wa mapinduzi
Image: REUTERS

Waziri Mkuu wa Sudan Minister Abdalla Hamdok ametangaza kujiuzulu wiki chache baada ya kurejeshwa madarakani katika mkataba wenye utata na majeshi.

Wanajeshi walichukuwa madaraka Mwezi Oktoba na kumweka Bw.Hamdok chini ya kifungo cha nyumbani, lakini akarejeshwa madarakani baada ya kufikia mkataba wa kugawana na kiongozi wa mapinduzi.

Waandamanaji walipinga makubaliano hayo, wakishinikiza utawala kamili wa kisiasa na kiraia.

Kujiuzulu kwake kunafuatia siku nyingine ya maandamano, ambapo madaktari walisema takribani watu wawili waliuawa.

Katika hotuba iliyooneshwa kwenye televisheni,Bw. Hamdok alisema Sudan iko katika "kipindi hatari ambacho kinatishia ustawi wake kwa jumla ".

Alisema alijaribu kila awezalo kuzuia nchi "kutumbukia kwenye janga ", lakini "licha ya yote yaliyofanywa kufikia uwiano... hilo halijafanyika ".

Waandamanaji wanaounga mkono demokrasia walikabiliwa na msako mkali kutoka kwa jeshi
Waandamanaji wanaounga mkono demokrasia walikabiliwa na msako mkali kutoka kwa jeshi
Image: GETTY IMAGES

" Niliamua kurudisha jukumu hilo na kutangaza kujiuzulu uwaziri mkuu, na kutoa nafasi kwa mwanaume au mwanamke mwingine wa nchi hii adhimu ili... kuisaidia kupita kile kilichosalia cha kipindi cha mpito kwa nchi kuelekea utawala wa kidemokrasia ya kiraia," aliongeza kusema.

Viongozi wa kijeshi walikubali shingo upande makubaliano ya kugawana madaraka yaliyolenga kupeleka nchi katika utawala wa kidemokrasia kufuatia maandamano makubwa yaliyochangia kuondolewa madarakani kwa rais wa muda mrefu wa Sudan Omar al-Bashir mwaka 2019.

Chini ya mkataba uliyofikiwa na Bw. Hamdok mwezi Novemba, waziri mkuu aliyerejeshwa madarakani alitakiwa kuongoza baraza la mawaziri hadi uchaguzi utakapofanyika. Lakini haikubainishwa utawala mpya wa kiraia utakuwa na uwezo kiasi gani, na waandamanaji walisema kuwa hawataki wanajeshi.

Maelfu ya watu walimiminika katika barabara za mji mkuu Khartoum na mji wa Omdurman siku ya Jumapili. Waandamanaji waliimba "madaraka kwa raia" na kutoa wito kwa jeshi kuachana na siasa.

Katika mitandao ya kijamii, wanaharakati wamesema 2022 itakuwa "mwaka wa kuendelea kwa upinzani".

Zaidi ya watu 50 wameuawa kwenye maandamano tangu mapinduzi hayo, ikiwa ni pamoja na angalau wawili siku ya Jumapili, kulingana na Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan wanaounga mkono demokrasia.

Kiongozi wa mapinduzi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametetea mapinduzi ya Oktoba mwaka jana, akisema jeshi lilichukua hatua ya kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa vinatishia kuzuka. Anasema Sudan bado inajitolea kwa mpito kwa utawala wa kiraia, na uchaguzi umepangwa kufanyika Julai 2023.

Uchambuzi

Januari 1 iliadhimisha Siku ya Uhuru wa Sudan lakini kuna mambo machache ya kusherehekea nchini humo kwa sasa.

Kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Abdalla Hamdok ni pigo kubwa kwa viongozi wa kijeshi ambao walidhani makubaliano na Bw Hamdok yangewaridhisha waandamanaji na kuhalalisha kusalia kwao mamlakani.

Ni wazi mahesabu hayo hayakuwa sahihi. Lakini ina maana kwamba jeshi sasa liko madarakani, na hivyo kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana wakati nchi hiyo ilipojaribu kurejea katika utawala wa kiraia.

Mgogoro wa sasa wa kisiasa unatishia kuirejesha Sudan katika miaka ya utawala wa kimabavu wa kiongozi wa zamani aliyeondolewa madarakani Omar Al Bashir.