Rais Samia apuuzilia mbali madai ya kumuambukiza Kamala Harris virusi vya Corona

Muhtasari

•Muda mfupi baada ya Samia kukutana na Kamalla vyombo vya habari vya Marekani vilitangaza kuwa amepatikana na Corona mbali na kuwa amepata chanjo zote.

Rais Samia katika mkutano wake na Kamala Harris
Rais Samia katika mkutano wake na Kamala Harris
Image: BBC

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amekanusha taarifa za kumuambikiza makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris virusi vya Corona.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru kwa vyombo vya habari jiji Arusha, Rais Samia amelazimika kusema hayo katika kukemea vitendo vya baadhi ya waandishi wa Habari kutoa kipaumbele kwa taarifa zisizo na umuhimu na ukweli.

"Wakati nilipokuwa Marekani waliandika kuwa, Mama yenu amepokelewa na Makamu wa Rais, lakini tena wakasema nimepata ugonjwa wa Uviko-19 wakiweka picha mtandaoni na kuweka mshale kwangu na yule Makamu wa Rais, nimepima kabla sijarudi, niko mzima" anasema rais Samia.

Mwezi uliopita rais Samia alifanya ziara ya kikazi nchini Marekani na kukutana na viongozi mbalimbali ikiwemo makamu wa rais wa Marekani Bi Kamala Haris.

Muda mfupi baada ya kukutana na Kamalla vyombo vya habari vya Marekani vilitangaza Kamala Harris kukutwa na Corona mbali na kuwa amepatiwa chanjo zote.

Licha ya kutoelezwa wazi kiongozi huyo ameambukizwa katika mazingira gani, makamu wa rais huyo wa kwanza mwanamke mweusi Marekani alikutwa na virusi hivyo Jumanne iliyopita. Lakini jana vipimo vimethibitisha kwa sasa amepona na hana virusi hivyo