Shambulio la Alshabab dhidi ya wanajeshi wa Burundi

Muhtasari

• Kundi la Kigaidi la al-Shabab limesema kuwa wao ndio wahusika kwenye mauaji makubwa katika shambulizi la katika kambi ya walinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia.

• Hata hivyo jeshi la Burundi limesema kuwa wanajeshi wake 10 ndio waliopoteza maisha na wengine watano waliopotea.

Jeshi la Umoja wa Afrika umekuwa Somalia tangu mwaka 2007
Jeshi la Umoja wa Afrika umekuwa Somalia tangu mwaka 2007
Image: AFP

Kundi la Kigaidi la al-Shabab limesema kuwa wao ndio wahusika kwenye mauaji makubwa katika shambulizi la katika kambi ya walinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, hata hivyo pande zote mbili zimekuwa zikitoa taarifa zinazokidhana juu ya idadi za vifo.

Kundi hilo ambalo ni washirika wa al-Qaeda wamesema wamewaua wanajeshi wapatao 170 wa AU, wengi wao wakiwa wametokea nchini Burundi pia kuwaweka mateka wengine bila kutaja idadi yao.

Hata hivyo jeshi la Burundi limesema kuwa wanajeshi wake 10 ndio waliopoteza maisha na wengine watano waliopotea.

Bado mpaka sasa hakuna taarifa za uhakika kuhusu shambulizi hili.

Kitu gani kilitokea kwenye shambulio hilo?

Mashambulizi hayo katika eneo la Shabelle ya Kati nchini humo yalishuhudia wapiganaji waliokuwa na silaha nzito wakivamia kambi ya al-Baraf kilomita 160 kaskazini-mashariki mwa mji mkuu, Mogadishu, ambako vikosi vya Burundi, vinavyohudumu chini ya AU, viliweka kambi.

Wananchi wa eneo hilo wanadai kusikia milio ya silaha nzito asubuhi.

"Shambulizi limetokea jana asubuhi,," Mjumbe wa AU, ambaye hakutaka kutambulika akiiambia BBC. "Magari mawili yaliyokuwa na mabomu na silaha yaliingia kwenye eneo na hapo ndio milio ya risasi ikaanza kusikika. Sifahamu idadi kamili ya waliopoteza maisha kwenye shambulizi lilitokea."

AU Inasemaje?

Umoja wa Afrika umelaani tukio hilo la kigaidi.

Mwenyekiti wa AU Moussa Faki Mahamat amesikitishwa na shambulizi hilo pia ametoa pole zake kwa askari waliofariki na kusema kuwa "Waliopoteza maisha hawatasahaulika kamwe".

Baada ya Uganda, Burundi pia ina washiriki wengi wa jeshi la Umoja wa Afrika nchini Somalia
Baada ya Uganda, Burundi pia ina washiriki wengi wa jeshi la Umoja wa Afrika nchini Somalia
Image: AFP

Katika taarifa iliyotolewa na AU inasema kuwa umoja huo hautarudishwa nyuma harakati za umoja ho katika kulinda amani nchini Somalia bali itaendelea mpaka itakapofanikisha lengo lake la kulinda amani.

Bwana Faki amesema kuwa amezungumza na Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye na kutoa rambi rambi zake.

Hatahivyo Rais Ndayishimiye amesema hakuna neno lenye nguvu zaidi ya kulaani mauaji ya wanajeshi walinda amani wa Burundi.

Jeshi la Burundi nalo limesema kuwa walinda amani 10 wameuwawa nchini Somalia na wengine watano wakiwa wamepotea, Mmoja wa kiongozi wa juu la jeshi la Burundi ameiambia AFP kuwa wanajeshi 30 ndio waliouliwa huku wengi wakiwa wamechukuliwa mateka.

Msemaji wa jeshi Luteni KanaliLt Daniel Mugoro Muiruri ameiambia BBC taarifa nyingi zinazotolewa sio za kweli bali watu wasubiri taarifa za uhakika.

AU huwa haitoi namba halisi ya watu waliouliwa kwenye shambulizi lililofanywa na al-Shabab.

Vipi kuhusu Somalia?

Serikali ya Somali nayo imelaani vikali shamblizi hilo lililotokea.

Imeitaka Atmis wakishirikiana na jeshi la Somalia kujilinda dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab.

"Tunatanguliza pole zetu kwa wahanga wa shambulizi la kigaidi, wa familia za marehemu, kwa Umoja wa Afrika na kwa washirika, Serikali na watu wa Burundi," Taarifa ya serikali ya Somalia.

Pia imetoa wito kwa mashirika ya kimataifa na nchi za magharibi kutoa msaada zaidi wa kupambana na ugaidi.

Al-Shabab huwa wanafanya mashambulizi kila mara Somalia
Al-Shabab huwa wanafanya mashambulizi kila mara Somalia
Image: GETTY IMAGES

Je, hili ni moja ya mashambulizi mabaya zaidi AU imepata?

Linatajwa kuwa ndio shambulio kubwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni, pia ni shambulio la kwanza kwa Atmis tangu kuchukua nafasi ya jeshi la zamani, linalojulikana kama Amisom.

Kikosi hicho kimsingi ni sawa na jina jipya lakini chini ya azimio la Umoja wa Mataifa, Atmis inapanga kupunguza polepole viwango vya wafanyikazi kutoka 20,000 hadi sifuri ifikapo 2024.

Kundi la Al-shabab linadhibiti kiwango gani cha ardhi ya Somalia?

Al-Shabab waliudhibiti mji mkuu wa Somalia Mogadishu hadi walipoondolewa na vikosi vya AU mwaka 2011.

Hata hivyo, kundi hilo la wanamgambo bado linadhibiti vijiji na maeneo mengi nchini humo, yakiwemo baadhi ya maeneo yanayopakana na mji mkuu. Pia inadhibiti njia kuu zinazoelekea jiji kuu.

Kundi hilo, linalotaka kuweka sheria kali za Sharia, au sheria za Kiislamu, mara kwa mara huwashambulia wanajeshi, raia na maafisa wa serikali katika mji mkuu na kote nchini humo.

Shambulio la hivi punde linakuja chini ya wiki moja baada ya bunge la Somalia kuwachagua maspika wa bunge - hatua ambayo inaifanya nchi hiyo kujiandaa na uchaguzi naokuja ambapo Bunger ndio litakalo chagua Rais ajaye.

Mchakato huo umezongwa na mzozo kati ya rais wa nchi hiyo na waziri mkuu, na kufanya wanamgambo hao kutumia mwanya huo.